Mpango: Ndugai ameacha somo familia duni si kikwazo uongozi

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameacha somo kwa jamii kuwa kuzaliwa katika familia duni si kikwazo cha kushika nafasi za juu za uongozi.
Dk Mpango alisema hayo wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Ndugai katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana.
Alisema Ndugai alizaliwa katika familia duni lakini hakukata tamaa ya kupambania ndoto zake hadi kufikia hatua ya kuongoza mhimili wa Bunge akiwa Naibu Spika na baadaye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Alikuwa mtu aliyelelewa katika mazingira ya kimaskini lakini haikumzuia kupanda juu kabisa mpaka kuwa mhimili wa Bunge na alisema hili mwenyewe mara kadhaa akihimiza watu wafanye kazi,” alisema Dk Mpango.
Aliongeza: “Kutoka familia masikini si kizuizi cha wewe kufika juu kabisa katika utumishi na hili lilikuwa funzo kubwa sana”.
Dk Mpango alisema Ndugai alikuwa akipenda kuona watu wakifanya kazi kwa bidii na kuweka utani kidogo katika kazi ili watu wafurahi.
“Wakati fulani Yanga iliifunga Simba basi tulikuwa na burudani kubwa kweli pale bungeni muda mwingine tuweke kidogo kazi na dawa ili mambo yaende,” alisema.
Dk Mpango alisema alimfahamu kwa ukaribu Ndugai yeye (Dk Mpango) alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na kuingia bungeni kwa mara ya kwanza na alimuelekeza mambo mbalimbali kuhakikisha kiasi cha fedha kinachopatikana kinatumika ipasavyo na kunufaisha taifa.
“Alikuwa kiongozi mahiri ambaye kila mara tulipokuwa katika kamati aliniongoza namna ya kuhangaika na keki ndogo ya taifa katika mahitaji mengi,” alisema.
Dk Mpango ametoa pole kwa Bunge la Tanzania, familia ya marehemu, wananchi wa Kongwa, wananchi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla.