Sheria ya uchaguzi inavyosisitiza umuhimu wa kudumisha amani, utulivu

SHERIA ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 inaelekeza namna ya kudumisha na kuenzi amani na utulivu kipindi chote cha kampeni, siku ya uchaguzi hadi matokeo kutangazwa.

Kwenye Kifungu cha 73 (4) cha sheria hiyo kinasema kwa madhumuni ya kuhakikisha amani na utulivu katika mikutano wakati wa kipindi cha kampeni, msimamizi wa uchaguzi ataitisha mkutano wa wagombea wote au
mawakala wa vyama na kupitia ratiba za kampeni za wagombea wote na kama italazimu kuwashauri wagombea kufanya mabadiliko katika ratiba zao kwa lengo la kuepuka migongano ya mikutano.

Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi ambao ndio wapigakura wanapata wakati mzuri na wa kutosha kusikiliza hoja na ajenda za vyama na wagombea wao ili wapate nafasi ya kufanya uamuzi ya kuchagua mgombea na chama chenye hoja na ahadi za kuvutia.

Ikiwa kutatokea migongano ama ya bahati mbaya au ya kukusudiwa itawasababisha wananchi kushindwa kupata nafasi ya kusikiliza hoja za wagombea na ahadi zao za namna watakavyotatua changamoto mbalimbali za kijamii na kuwaletea wananchi maendeleo.

Katika kuliratibu hilo vizuri, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024, Kifungu cha 73 (5) kinaeleza kuwa kila msimamizi wa uchaguzi atawasilisha nakala ya ratiba iliyoratibiwa kwa mkuu wa wilaya na mkuu wa polisi wa wilaya katika jimbo au kata na ratiba hiyo itachukuliwa kuwa ni taarifa ya mikutano inayopendekezwa kwa madhumuni ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Jeshi la Polisi na huduma saidizi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima anasema uwepo wa amani na utulivu unaenda sambamba na umakini kwa umma katika matumizi ya mitandao ya kijamii pamoja na utii wa sheria za uchaguzi kwa wagombea pamoja na vyama vyao katika kipindi chote cha uchaguzi.

“Nawasisitiza Watanzania na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa kuepuka matumizi mabaya ya akili unde ambayo inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu ya kusambaza habari za upotoshaji kupitia mitandao haswa ya kijamii,” anasema Kailima wakati wa kikao na wanahabari mkoani Dar es Salaam hivi karibuni.

Anaongeza kuwa ingawa mitandao ya kijamii ni chanzo muhimu cha habari na elimu kwa kuwa taarifa zinapatikana na kusambaa kwa urahisi na kwa haraka, kama waandishi hawatakuwa makini na kuweka taarifa za kweli na za uhakika zisizo na hata chembe ya upotoshaji nchi itapata taarifa muhimu zitakazolifanya taifa kuwa salama muda wote wa uchaguzi.

Wakili wa kujitegemea, Twarah Yusuph anasema sheria imeweka utaratibu huo ili kuondoa muingiliano wowote wa vyama na wagombea wao ndiyo maana ikamwelekeza mkuu wa wilaya na jeshi la polisi kuwa kwenye nafasi ya kufanya marekebisho ya ratiba pale kutakapotokea mgongano au muingiliano wowote.

“Bila kujali kifungu kidogo cha (5), mikutano ya hadhara haitafanyika katika jimbo au kata kwa madhumuni ya kuwezesha kampeni za uchaguzi za mgombea katika siku yoyote ya uchaguzi au pale ambapo siku mpya ya uchaguzi imepangwa kwa mujibu wa kifungu cha 71 (2),” inasema sehemu ya Sheria hiyo ya Uchaguzi katika ukurasa wa 67.

Wakili huyo anavitaka vyama vya siasa pamoja na wagombea wao kufuata sheria na kanuni za uchaguzi ili kuepusha migogoro isiyokuwa na ulazima inayoweza kwa kiasi kikubwa kuhatarisha amani na utulivu wa nchi kipindi hiki cha uchaguzi.

Masharti mengine yanayolenga kuleta utulivu wa nchi wakati wa kampeni hadi siku ya uchaguzi ni Kifungu cha 73. (1), kinachoeleza kuwa endapo kuna uchaguzi unaoshindaniwa katika jimbo au kata, kampeni za uchaguzi zitaendeshwa na mgombea, chama chake au wakala wake pekee.

Wakili Twarah anaishauri Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhakikisha sheria inafuatwa kikamilifu ili kuweka heshima kwa sheria mbalimbali za nchi na kuhakikisha zinafuatwa kikamilifu.

Sambamba na hilo, anasema sheria hiyo inaelekeza kuwa mgombea, wakala wake au chama chake cha siasa, kadiri itakavyokuwa, awasilishe kwa msimamizi wa uchaguzi mapendekezo ya ratiba inayoonesha mpangilio unaopendekezwa wa kufanya mikutano ya hadhara ya kampeni ya mgombea akiainisha muda na mahali mikutano itakapofanyika.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Gabriel Mwang’onda anasema wanasiasa na vyama vyao bila kuwekewa sheria na kulazimishwa kuzifuata ni rahisi kuliingiza taifa katika matatizo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mgombea, wakala wake au chama cha siasa kwa idhini au ridhaa ya mgombea anaweza kuitisha na kuhutubia mkutano wowote wa hadhara katika jimbo au kata utakaofanyika kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2), kwa lengo la kumwezesha mgombea kuchaguliwa au kuendesha kampeni za hadhara au nyumba kwa nyumba.

Mwang’onda anataja matarajio yake kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, utoaji wa kauli za vitisho, matusi na kutofuata utaratibu uliowekwa na INEC yatapungua kutokana na uimarishwaji wa kanuni na sheria za uchaguzi.

“Chaguzi nyingi zilizopita aghalabu wagombea na vyama husika wamekuwa wakifanya mambo na kusema maneno yanayohatarisha amani ya nchi lakini kwa uwepo wa sheria na kanuni za uchaguzi mkuu kwa kiasi kikubwa hali hiyo itapungua kwenye uchaguzi huu,” anaongeza Mwang’onda.

Kulingana na Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025, INEC katika kutekeleza majikumu yake ya kusimamia uchaguzi itasimamia Katiba ya nchi, Sheria ya INEC ya mwaka 2024 na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

INEC kupitia mwongozo huo inasema matumizi ya sheria hizo kwa kiasi kikubwa yanawahakikishia Watanzania kuwa haki itatendeka na amani na utulivu wa nchi utakuwemo mpaka wakati na baada ya kutangazwa kwa matokeo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button