Yanga, Dodoma Jiji wakwama kupiga kura TFF

TANGA; YANGA ya Dar es Salaam ni miongoni mwa klabu tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizokosa sifa ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unaofanyika Tanga asubuhi hii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Kiomoni Kibamba, aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa taratibu za uchaguzi zinaeleza kwa wanachama wa TFF upande wa klabu, mpiga kura atakuwa Mwenyekiti na wala si mtu mwingine. Kutokana na hali hiyo Yanga imekosa sifa hiyo kwani imewakilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Rodgers Gumbo.
Klabu nyingine ambazo pia zimekosa sifa hiyo ni Kagera Sugar na Dodoma Jiji. Pia wapo wajumbe wanne kutoka vyama tofauti vya mikoa nao wamepoteza sifa kutokana na kuwa wawakilishi na kufanya idadi ya wapiga kura halali kuwa 76 badala ya 83.
Licha ya kukosa sifa ya kupiga kura, lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, alisema wanayo sifa ya kuwa wajumbe wa mkutano huo kama wengine.



