Watu 9 mbaroni kwa utapeli mitandaoni

MBEYA; JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za utapeli na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook na WhatsApp.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti Agosti 18, katika mitaa ya Nsalala na Mapelele iliyopo Kata ya Nsalala, mji mdogo wa Mbalizi.

Watuhumiwa wanne kati ya hao walikuwa wanawadanganya watu kupitia mitandao hiyo kuwa wanatafuta wafanyakazi wa kuuza duka la jumla liitwalo Kajala lililopo Dar es Salaam.

Aidha, watuhumiwa wengine watatu walikuwa wakitumia simu zao kuomba fedha kwa watu wakidai wao ni wafanyabiashara wa kuuza bidhaa mbalimbali kwa bei rahisi maarufu “Tuma kwenye Namba hii”.

Vilevile watuhumiwa wawili wafanyabiashara walikamatwa wakijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kuwarubuni na kuwachangisha fedha watu mbalimbali ili wajiunge na kuwa wamiliki wenza wa kampuni ijulikanayo Q NET ya nchini Malaysia.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja Nemia Njonga (23) fundi rangi, mkazi wa Mwakapangala, Ombeni Ambilikile (22) dereva bodaboda, mkazi wa Nsalala, Jacob Peter (23) fundi rangi mkazi wa mwakapangala na Baraka Mgala (22) dereva bodaboda na mkazi wa mtaa wa Mbalizi.

Wengine ni mkazi wa Mbalizi, Lusajo Jeremiah (45), Adili Mbeyale (19) mkazi wa Mbalizi pamoja na Shaban Yasin (23) mkazi wa mtaa wa mshikamano, Ester Kimaro (28) mfanyabiashara na mkazi wa Nzovwe pamoja na Abdi Awadhi (21).

Alieleza kuwa watuhumiwa wamekuwa wakitengeneza viungo vya kughushi kwenye mitandao hiyo na kuwa mtu anayeomba ajira hutumia kujiunga kwenye kundi hilo na kisha hutumiwa ujumbe unaomtaka kutuma wasifu wake pamoja na fedha za kujaziwa fomu na kulipia sare za kufanyia kazi.

“Watuhumiwa wamekutwa wakiwa na simu mbalimbali pamoja na laini za simu za mitandao mbalimbali zilizosajiliwa kwa majina ya watu tofauti ambazo hutumika kupokelea fedha na kufanyia mawasiliano,” alisema Kuzaga.

Wakati huo huo, Jeshi hilo kwa kushirikiana na Askari wa wanyamapori (TAWA) kutoka Mpanga Kipengele linamshikilia Frank Alon (49) mkazi wa Uyole jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana meno manane ya tembo yenye uzito wa kilogramu 31.6 bila kibali.

Mtuhumiwa alikamatwa Agosti 17 mwaka huu katika Kijiji cha Nsonyanga kilichopo Kata ya Mahongole, Wilaya ya Mbarali akisafirisha meno hayo kwa kutumia usafiri wa pikipiki yenye namba za usajili MC 165 DDF aina ya TVS akiwa katika harakati za kutafuta mteja.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maofisa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linamshikilia Ikupa Mwakibibi (32) mjasirimali na mkazi wa Sae jijini Mbeya kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya shirika hilo kwa kujiunganishia umeme kinyume na utaratibu wa shirika hilo.

Mtuhumiwa alikamatwa Agosti 18, katika oparesheni za pamoja za jeshi la polisi, Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Tanesco ambapo baada ya kupekuliwa katika nyumba yake alikutwa akiwa na mita za umeme 19, rimoti za Tanesco 45 pamoja na waya rola 25.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button