Samia apongeza walioteuliwa kugombea

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amepongeza wanachama walioteuliwa kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani.

“Ninawatakia kila la kheri katika maandalizi ya safari yenu ya kwenda kuomba ridhaa ya wananchi kupitia sanduku la kura, kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025. Mwenyezi Mungu awatangulie, awaongoze na kuwafanikisha,” ameandika Rais Samia kwenye ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa X.

SOMA: CCM kuamua wagombea ubunge kesho

Agosti 23, mwaka huu Rais Samia aliiongoza Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa kufanya uamuzi huo, Dodoma.

Walioteuliwa wakiwemo wanawake 35 wataiwakilisha CCM katika uchaguzi wa wabunge kwenye majimbo 272 Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika kikao hicho cha NEC, CCM iliteua wabunge viti maalumu kupitia mikoa na makundi.

Miongoni mwa walioteuliwa hawakushinda katika kura za maoni lakini CCM imewapa fursa ya kugombea wakiwemo Ester Bulaya (Bunda), Esther Matiko (Tarime Mjini), Margaret Sitta (Urambo) na aliyekuwa mbunge wa Mufindi Kaskazini, Exaude Kigahe.

Pia, baadhi ya watia nia walioongoza kwenye kura za maoni lakini hawakupitishwa kugombea akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu na Priscus Tarimo (Moshi Mjini).

Wengine ambao walioongoza kura za maoni lakini majina yao hayajarudi ni watoto wa mawaziri wakuu wastaafu ambao ni Samwel Malecela (Dodoma Mjini) na Fredrick Lowassa (Monduli).

Wateule hao wanapaswa kwenda kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo kuchukua fomu za uteuzi na kazi hiyo itasitishwa Agosti 27.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeeleza wanapaswa kufika katika ofisi za wasimamizi wa uchaguzi wakiwa na barua za utambulisho kutoka katika vyama vyao kuanzia saa moja na nusu asubuhi hadi saa kumi kamili jioni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button