SIKU YA PAPA POTWE DUNIANI; WWF inavyoimarisha uhifadhi Mafia

AGOSTI 30, kila mwaka dunia inaadhimisha Siku ya Papa Potwe duniani ikiwa na lengo kuibua ufahamu na kuelimisha umma kuhusu samaki huyo na kuhamasisha juhudi za uhifadhi ili kumkinga na upotevu.
Siku hii ilianzishwa rasmi mwaka 2008 katika Mkutano wa Kimataifa wa Papa Potwe na wataalamu na wanaharakati zaidi ya 40 wa masuala ya bahari.
Samaki huyu anaelezwa kuwa ndiye mkubwa kuliko samaki wote baharini, ingawa anazua mjadala wa ukubwa baina yake na nyangumi, lakini ukweli ni kuwa papa potwe anabaki kuwa samaki mkubwa kuliko wote kwa sababu nyangumi hayuko kwenye kundi la samaki bali mamalia.
SOMA: ‘WWF iwezeshe jamii kiuchumi kukabili uharibifu wa mazingira’
Katika ukurasa wa mtandao wa X wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) sifa kubwa ya papa potwe inaelezwa kuwa ni samaki mpole na mkarimu.
Mtandao wa Wildlifetanzania unabainisha kuwa papa potwe anaweza kukua na kufikia urefu wa futi 18 hadi 32.8 na anauzito wa wastani wa tani 20.6 huku ikielezwa kuwa anaweza kuishi kwa miaka 70 kama atakuwa chini ya uangalizi wa binadamu.

Mtandao huo unaeleza kuwa papa potwe tofauti na samaki wengine wakubwa, yeye hula dagaa na vimelea ambao huingia mdomoni mwake na kuchujwa. Hata hivyo samaki hao wamekuwa katika changamoto ya uharamia wakikumbana na majeraha kutoka kwa wavuvi na wakati mwingine kuvuliwa na kuuawa.
Hayo yanasababisha kizazi cha samaki huyo kupungua duniani na hali inayofanya wadau na taasisi mbalimbali za uhifadhi hasa wa viumbe bahari kufanya jitihada za kulinda vizazi vya papa potwe. Hapa Tanzania papa potwe wanapatikana kwa wingi katika Wilaya ya Mafia, Kisiwa cha Mafia, mkoani Pwani kilometa 195 Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam.
Kufikia mwaka 2019 idadi ya papa potwe katika eneo la Mafia ilikuwa inapungua na kutishia uendelevu wa kizazi chao hapo ndipo WWF inachukua hatua za makusudi za kumlinda samaki huyo katika eneo la Mafia. Pamoja na mambo mengine WWF imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za kisayansi na kijamii ili kuboresha hali ya uhifadhi wa papa potwe.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya mwaka 2024 uliofanywa na WWF kwa kushirikiana na taasisi ya Marine Megafauna Faoundation idadi ya papa potwe imekuwa ikiongezeka na kushuka kati ya mwaka 2018 hadi 2024.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa idadi ya papa potwe imeongezeka kutoka 156 mwaka 2019 hadi 252 mwaka 2024 huku mapato ya nchi yakiongezeka kutoka Sh 53,207,500 mwaka 2018 hadi Sh 121,125,000 mwaka 2024. Aidha, idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 2,128 mwaka 2018 hadi watalii 5,044 mwaka 2024.
Hayo ni mafanikio yanayotokana na WWF kwa kushirikiana na wadau wengine wa uhifadhi wa mazingira kufanya juhudi za kuelimisha jamii ya mafia na kuwashirikisha katika uhifadhi wa papa potwe.
Akizungumza kuhusu maadhimisho ya papa potwe ya mwaka huu yanayoongozwa na ujumbe unaosema ‘Tunza mazingira ya bahari kumlinda papa potwe’, Msimamizi wa Mradi wa Uhifadhi wa Papa potwe wa WWF katika wilaya ya Mafia, Zephania Arnold anasema yanalenga kuendelea kujenga ufahamu miongoni mwa jamii ili kuwa na uhifadhi endelevu wa vizazi vya samaki huyo.
Anasema maadhimisho hayo yanayoshirikisha wana jamii ya Mafia wote wakiwemo wanafunzi yanalenga kuhakikisha usalama na ongezeko la papa potwe katika eneo hilo. “Tunataka kuinua ufahamu, kuhakikisha kila mtu Mafia anaufahamu na Papa potwe,” anasema Zephania.
“Tumekuwa tukifanya matembezi na wanafunzi na wavuvi. Tunataka watoto wajue kwamba wana wajibu wa kuwalinda.” Anasema katika maadhimisho ya kila mwaka wamekuwa wakishirikisha wanafunzi kwa sababu wanataka wajue wana wajibu wa kuhifadhi papa potwe tangu wakiwa wadogo.

“Tunachofanya katika kushirikisha wanafunzi ni kuhakikisha wanapata ‘knowledge’ (uelewa) wakiwa wadogo,” anasema. Anasema katika maadhimisho mwaka jana walifanya matukio mbalimbali ikiwemo matembezi ya hiari yakiwa yamebeba ujumbe wa ‘Tumlinde papa potwe, tulinde uchumi wa Mafia’, ili kuwaonesha umuhimu wa papa potwe kwa uchumi wa Wilaya mafia na visiwa vyake.
Anazitaja shughuli zitazofanyika katika maadhimisho ya mwaka huu kuwa ni pamoja na kusafisha fukwe, michezo mbalimbali kama kuogelea, mashindano ya majahazi, mashindano ya nyimbo na ngoma. Naye Mdau wa uhifadhi wa papa potwe katika Kisiwa cha Mafia, Emmanuel Msuya anasema WWF imekuwa ikifanya jitihada za kuibua uelewa juu ya uhifadhi wa papa potwe kwa watumiaji wa bahari na jamii ya Mafia.
Anasema WWF imefanikisha kuanzishwa kwa klabu za uhifadhi katika shule za msingi tano na za Sekondari tatu katika Wilaya ya mafia zenye takribani wanachama 1,500. Anasema mbali na hayo wanafanya tafiti kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuona idadi, changamoto zinazowapata ikiwemo majeraha, ustawi na ulinganisho papa potwe wanaopatikana Mafia na maeneo mengine.
Pia, anasema wanafanya tafiti kujua jamii inawachukuliaje papa potwe na inazungumza nini kuhusu samaki huyo.