‘WWF iwezeshe jamii kiuchumi kukabili uharibifu wa mazingira’

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira, Dk Ashatu Kijaji ameliomba Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) liwezeshe jamii kiuchumi kukabili uharibifu wa mazingira.

Ametoa ombi hilo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Sera na Utetezi wa WWF Dk Lin Lin katika kikao pembezoni mwa Mkutano wa Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi wa Uhifadhi wa Mazingira unaofanyika Cali, Colombia.

Advertisement

Dk Kijaji ambaye ameambatana na Ujumbe wa Tanzania, amesisitiza kuwa ni muhimu jamii iwezeshwe kukabiliana na visababishi vya uharibifu wa mazingira.

“Kama tunavyofahamu jamii inakabiliwa na changamoto ya kipato cha chini hivyo ni wakati muafaka sasa kwa shirika hili kuwekeza ili wananchi wetu waweze kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira,” amesema.

SOMA: Wajipanga kujadili changamoto za mazingira

Aidha, Dk Kijaji ametumia nafasi hiyo kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na shirika hilo nchini Tanzania katika kuhifadhi mazingira katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwa upande wake Dk Lin ameipongeza Tanzania kwa kuandaa Shabaha za Kitaifa za Kuhifadhi Bioanuai ambazo zitakuwa na mchango mkubwa katika kupunguza uharibifu wa bioanuai.

Sanjari na hilo pia ametoa pongezi kwa Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kutunga Kanuni za kudhibiti matumizi mifuko ya plastiki mwaka 2019 ambazo zinasaidia kukabiliana changamoto ya mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku nchini.

Hata hivyo, Dk Lin ameiomba Tanzania kuongeza ushawishi wa kimataifa na msukumo katika majadiliano ya kimataifa yanayoendelea duniani katika kuanzisha Mkataba wa Kimataifa kuhusu udhibiti wa matumizi ya plastiki (Intergovernmental Negotiation Commitee on Plastic, ICNP).

Waziri Dk Kijaji yupo Colombia akishiriki Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi wa Uhifadhi wa Mazingira uliotarajiwa kuhitimishwa Novemba Mosi.