Mfumo ufuatiliaji miradi kuanzishwa kudhibiti rushwa

MGOMBEA Mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi kuwa serikali ijayo ya chama hicho, itaanzisha mfumo wa ufuatiliaji miradi wenye lengo la kudhibiti mianya ya rushwa na ubadhirifu ikiwa itashinda Uchaguzi Mkuu 2025.

Dk Nchimbi ameyasema hayo akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika Kijiji cha Ngudu, Kata ya Mwankulwe katika Jimbo la Kwimba mkoani Mwanza.

Amesema mfumo huo ni miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030, lengo likiwa ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kikamilifu na kudhibiti mianya ya
rushwa na ubadhirifu.

SOMA: Nchimbi awasili Mwanza kampeni uchaguzi mkuu

Dk Nchimbi amesema nguvu kubwa zimewekwa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo nchini kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wake zinatumika ipasavyo na kwa ufanisi unaokusudiwa.

Amebainisha tangu Samia Suluhu Hassan alipokula kiapo cha kulinda amani na uhuru wa nchi, amejitahidi kwa nguvu kuhakikisha dhamira hiyo inasogea sambamba na uimarishaji wa maendeleo.

Aidha, amesema miradi imekuwa mingi kiasi cha kuleta changamoto pale inapochelewa kukamilika, jambo ambalo huibua malalamiko miongoni mwa wananchi, lakini Samia ameahidi kuikamilisha kwa muda uliopangwa ili kukidhi matarajio ya Watanzania.

Amesisitiza maendeleo ni kama jipu linalohitaji kusimamiwa kwa ukaribu na uadilifu, hivyo viongozi na wasimamizi wa miradi wanapaswa kuhakikisha kila hatua inatekelezwa kwa wakati bila kuruhusu mianya ya ucheleweshaji.

Ameongeza dhamira ya Samia ni kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili iende kwa mwendo mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa, hatua ambayo inalenga kuimarisha ustawi wa taifa na kuinua maisha ya wananchi.

Aidha, ametaja mambo mengine ambayo serikali ijayo inatarajia kuyafanya hususani kwa wananchi wa Kwimba kuwa ni kujenga zahanati mpya 20 na kukamilisha ujenzi wa zahanati nne unaoendelea, kujenga vituo vipya vya afya vitano na kuhakikisha Hospitali ya Wilaya ya Kwimba inakuwa na huduma zote za kibingwa.

Kuhusu elimu, amesema serikali hiyo itaendelea kuongeza madarasa katika shule za sekondari na msingi, kuongeza walimu na kuboresha zaidi mitaala.

“Tunataka watoto wetu wakaelimike. Tutahakikisha kila mtoto anaenda shule na ndani ya miaka yake mitatu anajua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK),” ameeleza.

Amerejea na kuwekea msisitizo ahadi aliyotoa mgombea urais kupitia chama hicho, katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika Kawe, Dar es Salaam kuhusu kuhakikisha makundi maalumu wakiwemo wazee, wajawazito, watoto na watu wenye ulemavu wanapata bima ya afya.

Kabla ya kutoa ahadi hizo, Dk Nchimbi alianza kwa kuelezea mafanikio lukuki ambayo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia imeyatekeleza hususani katika Wilaya ya Kwimba.

Amesema kwa upande wa afya, serikali imejenga Hospitali mpya ya Kwimba, kuongezeka kwa vituo vya afya kutoka 50 hadi 61 na idadi ya watumishi wa afya kutoka 335 hadi 513.

Kwa upande wa elimu, amesema shule za sekondari zimeongezeka kutoka 34 hadi 43, za msingi kutoka 154 hadi 161 na madarasa kutoka 436 hadi 709.

“Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kusema CCM haijafanya lolote. Na ukiona mtu anasema hivyo haraka sana muwahishe hospitali,” amesisitiza.

Amesema kwenye sekta ya maji upatikanaji umeongezeka kutoka asilimia 56 hadi 77, umeme hadi sasa vijiji 119
vimeunganishwa kutoka vijiji 60, barabara za changarawe kilometa 230 zimetengenezwa na za lami kilometa sita huku akiahidi kuwa zitajengwa za lami kilometa 120 ndani ya miaka mitano ijayo.

Dk Nchimbi amesema serikali ijayo itahakikisha wananchi wa Kwimba wanapata majisafi na salama kwa asilimia 90 na katika kilimo pembejeo, mbolea, dawa na mbegu zinapatikana kwa bei nafuu na masoko kupatikana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge amewataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Samia na wagombea wote wa CCM.

“Tunaingia kifua mbele tuna mtaji wa wanachama waliojisajili kwenye mfumo wetu zaidi ya 700,000. Tunakuhakikishia kura za Rais Samia zitakuwa ni za kutosha,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button