Waandishi watakiwa kuithibitishia dunia Tanzania ni nchi ya amani

MBEYA : SERIKALI imesema waandishi wa habari wana jukumu la kuithibitishia dunia kuwa Tanzania ni taifa lenye umoja, amani na utulivu.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Mbeya na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati wa mkutano wa wadau wa habari na utangazaji kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ulioshirikisha pia vyombo vya ulinzi na usalama.
Profesa Kabudi alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi, waandishi wa habari wanapaswa kuiarifu dunia kuwa Tanzania ni taifa linalojali maendeleo ya wananchi wake bila kujali dini, kabila au kipato.
“Waandishi wa habari muieleze dunia kuwa Tanzania ni nchi yenye watu waliokomaa kisiasa, wenye uwezo wa kuvumiliana na kushirikiana,” alisema Profesa Kabudi.
Mshikamano wa kitaifa
Alisema waandishi wamekuwa kiungo cha mshikamo wa taifa tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kuhakikisha Watanzania wanasimama pamoja hata wakati wa majanga. “Mnalo jukumu kubwa la kuwaelimisha wananchi kuhusu haki ya kujitawala na umuhimu wa taifa letu kama nchi huru yenye haiba, hulka, mila, desturi na mwelekeo wake,” alisema.
Amani na Ustahimilivu
Waziri huyo alisisitiza kuwa amani ya nchi ni msingi wa maendeleo na inatokana na ustahimilivu wa wananchi. “Ustahimilivu si udhaifu bali ni alama ya uzalendo. Mtu anayetoa kauli inayoweza kuvunja amani si mzalendo na hajui thamani ya amani,” alisema Profesa Kabudi na kuongeza kuwa msingi wa amani ni maelewano na majadiliano.
Ushirikiano na Vyombo vya Ulinzi
Profesa Kabudi alisema ushirikiano wa Jeshi la Polisi na vyombo vya habari katika maandalizi ya uchaguzi unaonesha dhamira ya serikali kukuza demokrasia, kudumisha amani, haki na uwajibikaji.
Alisema vyombo vya habari vina wajibu wa kuonesha na kulinda fahari ya maendeleo ya nchi kwa kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa za kimaendeleo.
“Moja ya kazi yenu hasa katika kipindi hiki ni kueleza mafanikio makubwa tuliyopata, kwa sababu hiyo ndiyo fahari ya taifa,” alisema.
Historia ya Uchaguzi
Akizungumzia historia ya chaguzi nchini, Profesa Kabudi alisema Tanzania imekuwa na utamaduni wa kufanya uchaguzi hata katika mazingira magumu, akitolea mfano mwaka 1980 ambapo licha ya shinikizo kubwa la kuahirisha uchaguzi kutokana na vita dhidi ya Idd Amini, bado uchaguzi ulifanyika.
Alibainisha kuwa tangu uchaguzi wa vyama vingi wa mwaka 1958 hadi 1962 na hata wakati wa chama kimoja kati ya 1965 hadi 1985, Watanzania waliendelea kuthibitisha mshikamo wao kwa sababu ya imani ya pamoja katika demokrasia.
“Vielelezo vya demokrasia ni wananchi kuwa na uwezo, haki na wajibu wa kuchagua viongozi wao kila baada ya kipindi fulani. Tanzania imeonesha mfano huo tangu enzi hizo,” alisema Profesa Kabudi.
SOMA: KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025: Kataa siasa za uchochezi, hoja za chuk



