Tusikilize sera kwenye kampeni, wavuruga amani tuwakatae

WAKATI siku za kampeni zikiendelea nchini wagombea na vyama vyao vya siasa wameshaanza kupanda majukwaani kunadi sera za vyama vyao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kampeni hizi zitazinduliwa na vyama vya siasa kwenye maeneo mbalimbali watakayoyapanga, lakini sharti vyama hivyo vinatakiwa kuwa vilithibitishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kushiriki mchakato mzima wa uchaguzi huo.
Mpaka sasa vyama 18 vyenye usajili wa kudumu ndivyo vyenye kibali cha kushiriki mchakato wa uchaguzi kuanzia kampeni na uchaguzi na vimeshawasimamisha wagombea wa nafasi ya urais, ubunge na udiwani. Vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Chama cha ACT Wazalendo, Chama Cha Kijamii (CCK), Chama cha MAKINI, United Peoples’ Democratic Party (UPDP) na National League for Democracy (NLD).
Vingine ni National Reconstruction Alliance (NRA), Tanzania Labour Party (TLP), Union for Multiparty Democracy (UMD), Tanzania Democratic Alliance (ADA-TADEA) na Alliance for African Farmers Party (AAFP). Kimo pia Chama cha Wananchi CUF, Chama cha NCCR-Mageuzi, Chama cha United Democratic (UDP), Chama cha Democratic Party (DP), Sauti ya Umma na Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Katika uchaguzi huo, idadi ya majimbo yatakayopigiwa kura ni 272 hii ni kutokana na ongezeko la majimbo mapya manane yaliyotangazwa na INEC ambapo majimbo 222 yakiwa Tanzania Bara huku 50 yakiwa Zanzibar. SOMA: Uchaguzi Mkuu 2025 kielelezo cha demokrasia EAC
Idadi ya wapigakura waliojiandikisha ni 37,655,559, Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 26.55 kutoka wapigakura milioni 29.7 waliokuwa wamejiandikisha katika daftari mwaka 2020. Ndugu zangu Watanzania, ninawiwa kuwaomba sana katika mchakato huu wa kuelekea uchaguzi mkuu, tukijitahidi sana kuikumbatia amani yetu ambayo ndio tunu ya taifa hili.
Twende kwenye viwanja vya kampeni kusikiliza sera wanazotoa wagombea, lakini tusiruhusu, chuki na siasa za kutugawa Watanzania.Ninawasisitiza sana tuwe makini kusikiliza sera za kila chama ili unaposhiriki uchaguzi Oktoba 29, ujue unamchagua nani atakayeweza kuisogeza jamii yako kimaendeleo.
Nirudi kwenu wanasiasa, ninaomba mfanye siasa safi kwenye majukwaa yetu, tusifanye siasa za kutugawa Watanzania na kuharibu amani ya taifa letu ambayo waasisi wetu waliipigania kwa hali na mali.
Ninashauri, baada ya kumaliza mchakato huu muhimu kwa mustakabali wa taifa letu tuvunje makundi, tushikamane, tuwape nafasi watakaopata ridhaa ya kutuongoza kutatua kero na kutuletea maendeleo kwenye maeneo yetu.
Ninasisitiza tusikubali, na asiwepo mtu yeyote kutoka ndani ya nchi au nje atakayesimama kuhamasisha kufanya vurugu za kutugawa na kuvunja amani yetu tukamsikiliza. Ninasema hivi kwa sababu wapo wasiolitakia mema taifa hili, tukumbuke kwenye machafuko wanaoathirika zaidi ni wanawake, watoto na wazee hivyo tusiruhusu hili litokee kwani kurejesha amani ni ngumu sana.
Tujifunze kutoka kwa nchi majirani zetu ambao walipata machafuko baada ya uchaguzi ikiwemo Kenya na Msumbiji ambako mamia ya watu walipoteza maisha huku mali zikiharibiwa vibaya.