Chama cha MAKINI kufuta mikopo ya elimu ya juu

CHAMA cha Demokrasia Makini (MAKINI) kimesema serikali yake itafuta mikopo ya elimu ya juu.

Mgombea urais kupitia chama hicho, Coaster Kibonde amesema hayo wakati akizindua kampeni za chama hicho kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, Manzese mkoani Dar es Salaam na akasema ahadi hizo atatekeleza ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa.

Amesema serikali ya Chama cha MAKINI itawapa wagombea urais wa vyama vyote nafasi lakini nafasi ya kwanza ndani ya muda mfupi atapewa Samia kwani amebaini amebobea kwenye diplomasia ya kimataifa, uchumi na siasa.

“Nitampa kazi Ikulu, nikishinda atabaki Ikulu afanye kazi kwenye madawati hayo, wengine mtanisubiria baada ya kubadili katiba na wagombea wote mtapata nafasi kwa sababu mna nia thabiti ya kuijenga nchi,” amesema
Kibonde.

SOMA: Makini kushiriki uchaguzi mkuu 2025

Ameongeza: “Vipaumbele vya Chama cha MAKINI ni vitatu; elimu, kilimo na afya. Tukipata ridhaa kuanzia
elimu ya awali hadi chuo kikuu elimu itakuwa bure hakuna kutoa mikopo, wanafunzi watasoma bure kwa
gharama za serikali popote duniani,” amesema.

Pia, Kibonde alisema wamebaini vijana wa Kitanzania wako zaidi ya milioni 20 na iwapo wananchi watampa ridhaa kupitia chama hicho kila kijana atapewa ekari tano bure.

“Vijana wengi hawaaminiki kwenye taasisi za benki kwa ajili ya kupewa mikopo hivyo kila ekari hizo tano zitapewa hatimiliki na kuwawezesha vijana kuzitumia kama dhamana katika taasisi za kibenki,” amesema.

Kibonde amesema Chama cha MAKINI kitaanzisha viwanda vitakavyozalisha malighafi zinazohusiana na
kilimo kama pembejeo na hivyo mkulima hatasubiria pembejeo ila pembejeo ndio zitamsubiri mkulima kwenye maghala.

Kuhusu afya, amesema watajenga hospitali kila kata nchini na kuwekwa vifaatiba. Kibonde alisema Serikali ya MAKINI imefanya mawasiliano na nchi mbalimbali na kugundua zina uhaba wa wafanyakazi hivyo chama hicho kitawatafutia vijana kazi katika mataifa hayo ili kuinua uchumi.

Mgombea mwenza wa urais kupitia chama hicho, Azza Haji Suleiman amehimiza Watanzania wadumishe umoja na amani na kusema bila uwepo wa mambo hayo kampeni zisingefanyika.

“Hivyo niwasihii vijana msikubali kurubuniwa ili mchochee vurugu, ukitowesha amani tambueni nyuma yenu mna wazazi, wagonjwa na wasiojiweza. Endapo amani itavurugika, hali haitakuwa nzuri,” alisema Suleiman.

Mgombea urais wa chama hicho upande wa Zanzibar, Ameir Hassan Ameir alisema kwa upande wa mamalishe chama kitaanzisha mfuko na akina mama watapewa mkopo na kurudisha bila masharti au riba.

Ameir ameahidi waendesha bodaboda kuwa kila Mtanzania kijana anayetaka kufanya biashara ya kuendesha bodaboda atapewa bure pikipiki na katika awamu ya kwanza zitatolewa pikipiki 1,000,000.

Amesema hakutakuwa na kutoa pikipiki kwa mkataba bali vijana watapewa bure. Ameir amesema Serikali ya MAKINI itatoa posho ya wazee kila mwezi na kwamba kila mzee atakuwa akipata Sh 100,000.

Kwa wafanyabiashara ya mitumba, kila mmoja ameahidiwa kupewa mtaji wa milioni 10 bila masharti yoyote.

Aidha, Ameir amesema sekta ya habari itaboreshwa na chama hicho kitawapeleka waandishi wa habari nchini Canada kuongeza ujuzi ili wafanye kazi kwa weledi zaidi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button