Mgombea upinzani amuunga mkono Dk Mwinyi

ZANZIBAR : MGOMBEA urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ADA TADEA, Juma Ali Khatib amesema anamuunga mkono mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi.

Khatib alisema hayo baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Kazi kumkabidhi fomu ya kuomba uteuzi. Aliwaeleza waandishi wa habari kwamba anamuunga mkono Dk Mwinyi kwa kuwa katika miaka mitano ameleta maendeleo kutokana na utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Tunamuunga mkono mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk Hussein Mwinyi ambaye namtakia ushindi na mimi nipate ushindi wa pili ili niwe makamu wa kwanza wa rais na hivyo kufanya kazi naye pamoja kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Zanzibar,” alisema Khatib.

Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman baada ya kuchukua fomu jana alisema chama hicho kimejipanga kushiriki uchaguzi. Othman alisema uchaguzi ni mfumo wa kidemokrasia unaotoa nafasi kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka kwa kutumia sanduku la kura.

“Chama cha ACT Wazalendo kipo tayari kwa uchaguzi mkuu ambao ndio utakaowapa wananchi nafasi ya kuchagua viongozi wao kwa njia ya kidemokrasia na hatuna sababu ya kususia uchaguzi huo,” alisema. Mgombea urais kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad baada ya kuchukua fomu jana alisema chama hicho kikishinda kitapambana na umasikini.

“Hiyo ndiyo sera yetu kuona kwamba wananchi wanaondokana na umasikini na kupiga hatua kubwa ya maendeleo ikiwemo ya kiuchumi,” alisema Hamad. SOMA: Vyama vyafundwa kupata wagombea

Mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya chama cha SAU, Ali Mwalimu Abdalla baada ya kuchukua fomu jana aliahidi kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar. Mgombea urais Zanzibar kupitia NCCR Mageuzi, Leila Rajab Khamis alisema ndoto yake ni kuinua uchumi wa Zanzibar.

“Nikichaguliwa nataka kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika nishati ya mafuta na gesi ili kuweza kuwainua wananchi kiuchumi na uwekezaji,” alisema Leila.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button