UMD yaahidi kutatua kero kubwa tano siku 100 Ikulu
MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Milambo amesema wamejipanga kutatua kero kubwa tano ndani ya siku 100 madarakani.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Milambo amesema anatambua kero kubwa zinazosumbua wananchi kwenye masuala ya afya, maji, elimu, miundombinu na sekta binafsi. Hivyo chama chake kimejipanga kuzitatua mapema.
“Hizo ndizo kero kubwa ambazo Watanzania wote zinatugusa, najua kuna wafanyabishara ndogondogo wana kero nyingi sana. Zote hizo, UMD imejipanga vizuri kuondokana nazo… Oktoba 29 Watanzania chagueni rais kutoka UMD hamtajutia,” amesema.
SOMA: Kumekucha kampeni za Uchaguzi Mkuu
Milambo amesema pia chama chake kinafahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana na wanawake.
Hivyo Watanzania wakiwachagua changamoto hizo zitakuwa historia. Amesema kupitia sera yao ya majimbo tutahakikisha kila mmoja ananufaika na rasilimali za nchini.
Amesema, “Mimi kama mzazi nasikitika sana ukipita mjini mahali kama Mnazi Mmoja unakuta kundi kubwa la watoto wadogo wanalala barabarani unawaona unalia, watoto wadogo masikini ambao wanatakiwa kuwa shule lakini wanalala mitaani, yaani suala la malezi siku hizi limekuwa kitendawili sana, watoto wanajilea wenyewe”.
Amesema endapo watatwaa nchi, serikali yake itahakikisha waliokuwa vijijini wanapata mafanikio hukohuko badala ya kukimbilia mjini.
“Tutahakikisha kila kitu kinafanyika kisasa na kwa weledi, waliokuwa vijijini kama wanalima basi iwe kilimo kitakachowasaidia. Hii maana yake, tutaweka mazingira wezeshi kulima kilimo cha kisasa, miundombinu iwe mizuri watafutiwe masoko, wakija mjini kuuza bidhaa zao wawe kamili kamili wakijua wanauza na wanapata
fedha,” amesema.
Ameongeza: “Siyo waje mjini kwa kubahatisha kwamba wanaweza kuuza ama wasiuze, wanatakiwa kuja mjini wakijua wanakwenda wapi na wanauzaje bidhaa zao.”
Amesema, “Ni utaratibu tu, naamini kwa mipango mizuri ya UMD tukipata nafasi ya kushika dola, mambo yatabadilika na uchumi ukiwa mzuri hapa hata ukimwambia mtu suala la uzalendo, haimchukui muda kuelewa… ndiyo maana kaulimbiu yetu kwenye uchaguzi huu tunasema ‘Chagua UDM, Chagua Mwajuma Noti Milambo’ hutojuta kuzaliwa Tanzania”.
Kuhusu kampeni, amesema chama chake kimejipanga vizuri na kinatarajia kuzindua kampeni zake keshokutwa Muheza, Tanga.
“Mimi na timu yangu tutakwenda kuzindua kampeni zetu Muheza, lengo kubwa ni kuzungumza na Watanzania na wanaMuheza kwamba yapo madini pale, tukijipanga yatakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania,” amesema.


