CCM yaja na Tume ya Maridhiano

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema wananchi wakimchagua mgombea wake wa urais, Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 itaundwa Tume ya Maridhiano.

Mgombea Mwenza wa Samia, Dk Emmanuel Nchimbi amesema tume hiyo itawaunganisha Watanzania wote, wananchi wote watasikilizwa, wachache na walio wengi ili taifa liendelee kuwa imara likiwa na upendo na mshikamano.

Dk Nchimbi amesema hayo katika mkutano wa kampeni Lalago wilayani Maswa mkoani Simiyu.

“Hakuna faida ya taifa lenye watu wanaovurugana na wasiosikilizana. Tume ya maridhiano italeta mshikamano na umoja wa nchi yetu, tutaondoa ubaguzi wa aina yoyote, ukabila, udini na itikadi ili kila mmoja ajivunie kuwa Mtanzania,” alisema.

SOMA: Uzoefu kuivusha salama Tanzania Uchaguzi Mkuu 2025

Aidha, amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia imekusudia kuanzisha mfumo mpya wa mawasiliano ya wananchi na viongozi kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa ili kurahisisha utoaji wa maoni na utatuzi wa changamoto.

Dk Nchimbi amesema dhamira hiyo inalenga kuendeleza urithi wa amani ulioachwa na waasisi wa taifa na kuifanya Tanzania iendelee kuwa kivutio cha wageni kutokana na mshikamano wake wa kijamii.

Katika mkutano huo wa mwisho mkoani Simiyu amesema maendeleo yaliyopatikana Maswa ni ushahidi wa utekelezaji wa ilani ya CCM.

Ametaja baadhi ya maendeleo hayo ni ongezeko la vituo vya afya kutoka vitatu hadi nane, zahanati kutoka 35 hadi 44, pamoja na ujenzi wa majengo mapya ya huduma za dharura na mionzi katika Hospitali ya Wilaya.

Dk Nchimbi amesema sekta ya elimu imeimarishwa kwa ongezeko la shule za sekondari kutoka 36 hadi 47, shule za msingi kutoka 125 hadi 135, huku miundombinu ya madarasa ikiboreshwa.

Katika maji, upatikanaji umeongezeka kutoka asilimia 63 hadi 77 kupitia miradi mikubwa yenye thamani ya Sh bilioni 20.8.

Amesema vijiji vyote 120 vya Maswa vimeunganishwa na umeme na pia sekta ya mifugo imenufaika kwa ongezeko la majosho kutoka 31 hadi 73 na maboresho ya minada ambayo yameongeza kipato cha wafugaji.

Dk Nchimbi amesema barabara zinazopitika sasa zimefikia kilometa 1,084 zikiwemo kilometa 4.8 zilizowekwa lami.

Amesema kwa miaka mitano ijayo, CCM imepanga kujenga vituo sita vya afya, zahanati 10, shule za msingi zenye madarasa mapya 100 na sekondari zenye madarasa 200, na maabara 75.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button