ADC kufuta malipo kumuona daktari

CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema serikali yake itafuta utaratibu wa mgonjwa kulipa fedha za kumuona daktari katika hospitali za serikali.

Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shaban Itutu amesema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika Pasiansi jijini Mwanza.

Amehoji: “Daktari ni mtumishi wa serikali na analipwa na serikali kupitia kodi zetu, kwa nini unapoenda hospitali kumuona unaambiwa ulipie kumuona? je, ni halali kutoa fedha kumuona mtu anayelipwa na serikali tena kwenye huduma za afya”?

Ameongeza: “Kwa uongozi wa ADC, huduma za afya zitakuwa ni bure kwa sababu watu wanakufa kwa kukosa huduma hizo kutokana na gharama zilizopo kuwa kubwa ili hali watu wake hawawezi kuzimudu.”

SOMA: ADC yaja na mikopo kwa wanaume, afya, elimu bure

Itutu amesema serikali ya ADC itahakikisha rasilimali za taifa zinatumika kuboresha huduma za jamii zikiwemo afya, maji na elimu.

Mwanasiasa huyo anayegombea ubunge katika Jimbo la Ilemela, ameahidi kuwa endapo ADC itaingia madarakani, bei ya mtungi wa gesi wa kilo 25 itashuka kwa kuwa gesi inapatikana nchini.

Pia, Itutu alisema serikali ya ADC itafuta ushuru kwa wajasiriamali wanaofanya biashara ndogo ndogo ili kusaidia familia zao.

“ADC tunataka mtu atakayelipa kodi aanze na mtaji wa Shilingi milioni tano tena pale atakapokuwa amekwishapata faida na biashara yake imekua na si vingine. Tutakuwekea utaratibu mzuri ili kupandisha uchumi. Haiwezekani mkawa masikini kila siku, kila siku mnanyanyaswa na mnanyang’anywa fedha zenu,” amesema.

Mgombea urais kupitia ADC, Wilson Mulumbe amesema kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa sekta ya elimu kwa kuajiri walimu wenye sifa, kuwalipa vizuri na kupambana na mifumo mibovu ya upatikanaji wa vyeti.

Mulumbe alisema atahakikisha anajenga nyumba mpya na za kisasa kwa ajili ya askari Polisi.

“Nimefanya utafiti nchi nzima nimegundua makazi yao si rafiki hivyo punde tu nitakapochaguliwa nitahakikisha na vunja nyumba zote zilizojengwa miaka 1980 nakujenga nyumba mpya za kisasa,” amesema.

Mulumbe amesema kipaumbele cha pili ni huduma za afya kutolewa bure na kukomesha biashara zote ikiwemo kuuza kadi, daftari na kwamba hakutakuwa na kununua dawa pale daktari anapomuandikia mgonjwa.

Amesema huduma za kuunganisha umeme zitatolewa bure nchi nzima.

Amesema hadi sasa ni asilimia 36 ya Watanzania wanatumia umeme kutokana na ukubwa wa gharama za kuunganishiwa huduma hiyo hasa mijini.

Mulumbe amesema huduma ya maji itatolewa bure kwa wananchi na serikali itatoza kiasi kidogo kila mwezi kulingana na gharama za wakati huo kwa ajili ya kulipia huduma za uzalishaji zaidi.

Amesema serikali ya ADC itafufua viwanda vya ndani huku ikiwekeza kwenye viwanda vipya ili kuongeza thamani ya mazao na kutoa ajira kwa vijana.

Mgombea mwenza wa Mulumbe, Shoka Juma alisema chama hicho kitaunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayoshirikisha vyama vyote badala ya chama kimoja pekee kushika nafasi zote za uongozi.

“Kwenye nafasi 10 za uteuzi wa rais, sisi tutahusisha vyama vingine vyote, ikiwemo CCM, ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika kuongoza nchi,” amesema Juma.

Aidha, amesema serikali ya ADC itaweka mfumo wa mikopo ya kijamii usio na riba, utakaowahusisha wanaume, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu bila ubaguzi.

“Mikopo ni muhimu lakini imekuwa ikitolewa kwa makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu lakini kundi kubwa la wanaume kuanzia miaka 25 mpaka 60 likisahaulika hili ndilo linalotegemewa katika familia zao na katika kujenga uchumi wa nchi kwa asilimia zote sisi tutatoa kwa kila mtu,” amesema Juma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button