Mjue kakakuona na maajabu lukuki

KAKAKUONA ni mnyama wa kipekee ambaye mwili wake umefunikwa na magamba kuanzia kichwani hadi mkiani wakiishi maisha ya upole kwa sababu mara nyingi mnyama huyo si wa vurugu wala madhara kwa watu.
Julai 6, 2025 chini ya kichwa cha habari: ‘Umewahi Kuona Aina Ipi ya Kakakuona Kati ya Hizi?’ Hillary Mrosso aliandika katika wildlifetanzania.co.tz kuwa, miongoni mwa spishi au aina 4 za kakakuona wanaopatikana Afrika, Tanzania ina aina 3 ambazo ni kakakuona wa ardhini, kakakuona tumbo jeupe na kakakuona mkubwa.
Anasema licha ya kuwa ni wanyama wasioonekana mara kwa mara, kakakuona wanapoonekana wanakuwa na mvuto na hisia kubwa katika jamii.
“Wengi huamini kakakuona ni mnyama anayekuja sehemu fulani kwa ajili ya kuleta ishara ya jambo fulani kwenye jamii. Hivyo, watu humuona kama mnyama wa kipekee sana na mwenye nguvu fulani tofauti na wanyamapori wengine,” anaandika Mrosso.
Anaongeza: “Kubwa zaidi, ni imani na tamaduni za jamii husika zinazohusishwa kwa mnyama huyu. Hivyo, kuna mengi hayajulikani kuhusu namna wanavyohusishwa kwenye mambo ya imani na ukweli wa mambo hayo kisayansi.” “…Ni wanyama ambao wana aibu sana na hawawezi kula au kuwa huru mbele za watu wengi au kwenye kelele, hivyo ukimkamata kakakuona ni vizuri akarudishwa porini haraka.”
Tovuti ya Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) inamwelezea kakakuona kama mnyama anayependa kufanya shughuli zake usiku. Hii ni kutokana na kinachosemwa kuwa maumbile yao yanawafanya watambulike kiurahisi kutokana na hali yake ya magamba.
SOMA: Mkulima Ihemi amkamata Kakakuona
Kwa kawaida, magamba hayo ni kinga kwake kwa kuwa anapohisi hatari, mnyama huyo huficha kichwa chake kwenye mikono yake na hata anapoguswa hujiviringa kama mpira na kujifunika kwa magamba hayo kujikinga dhidi ya hatari inayomkabili.
Kakakuona anaweza kuishi hadi kufikia miaka 20 na ukubwa wake huanzia sentimeta 30 hadi 152 huku uzito wake ukianzia kilo 1.5 hadi 33. Mfuko wa Wanyamapori Afrika (AWF) kupitia tovuti yake unabainisha kuwa, kakakuona pia hutumia magamba yake kama silaha ya kujikinga dhidi ya maadui.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, mtu au mnyama yeyote anapomkaribia na kutaka kumdhuru, kakakuona hutumia magamba yake kumbana kwa kuwa yana uwezo wa kumjeruhi mtu kwa kumkata.
Wakati mwingine, mnyama huyo adimu hutoa harufu mbaya na inayofanya baadhi ya wanyama wanaotaka kumdhuru kukaa mbali naye. Inaelezwa kuwa akiwa na mtoto, kakakuona wa kike humweka mtoto wake kwenye mkia, lakini inapotokea hatari mtoto huteleza kwenda chini kwenye mkia na mama yake kujikunja haraka kama mpira na kumfunika.
Kwa kawaida mnyama huyo hutumia muda mwingi wa mchana kujificha kwenye mashimo na kutoka usiku kutafuta chakula. Vyanzo kadhaa vinasema chakula kikuu cha kakakuona ni wadudu hususani mchwa ambao huwapata kwa kuchimba kwenye vichuguu kwa kutumia kucha ngumu alizo nazo zinazowasaidia kuchimba na kisha kuwala kwa kutumia ulimi wake mrefu unaoweza kufikia sentimita 41.
Makala iliyochapwa kwenye tovuti hiyo inaeleza kuwa, ulimi wa kakakuona ni mrefu kuliko mwili wake na kwa urefu huo, humrahisishia kupata mawindo (chakula).
Kwa nchi za Afrika mnyama huyo amekuwa akihusishwa na masuala ya kiutamaduni kutokana na tabia yake ya kupenda kujificha nyakati za mchana na kumfanya kuwa adimu kiasi kwamba, watu wamuonapo huamini ni kiumbe wa pekee anayeweza kuwasaidia hata kutatua matatizo yao.
Mwaka 2021 mnyama huyo alionekana katika Kijiji cha Wami Sokoine wilayani Mvomero katika Mkoa wa Morogoro. Kuonekana kwa kakakuona huyo kulizua hekaheka na kila mwanakijiji kumchukulia kwa maana anayojua yeye. Wanakijiji hao walitaka kumshika na kupiga naye picha, lakini wengine wakifika mbali zaidi kwa kumweleza matatizo yao ili awatatulie.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti la HabariLEO, zipo baadhi ya jamii ambazo kakakuona anapoonekana katika mazingira au maeneo yao, hucheza ngoma na kufanya matambiko ya kumzungushia unga na kumwekea maji huku wengine wakimwekea silaha kama panga, mkuki au jembe.
Pamoja na upekee wake na hata kujilinda kwake, kakauona amejikuta katika kundi la wanyama walio katika hatari ya kutoweka kutokana na kushamiri kwa biashara ya nyama na magamba yake. Tovuti ya AWF inabainisha kuwa, kakakuona anashika nafasi ya kwanza katika orodha ya mamalia wanaosafirishwa kwa magendo duniani.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhifadhi wa Mazingira limebaini kuwa, kati ya mwaka 2000-2019, karibu kakakuona laki 9 walisafirishwa. Kwa upande mwingine, mwaka 2019 mamlaka nchini Malaysia ilikamata tani 27 za nyama ya kakakuona.
Tovuti hiyo inaeleza kuwa, magamba ya kakauona yanaaminika kuwa na uwezo wa kuponya magonjwa kama saratani na kutoka damu puani. Hata hivyo, magamba hayo yanahusishwa pia na imani za kishirikina. Katika baadhi ya nchi za Afrika, inaaminika kuwa magamba ya kakauona yakichanganywa na magome ya baadhi ya miti hunazuia uchawi na mikosi.
Mbali na hayo yapo, makabila yanayoamini kwamba kuonekana kwa mnyama huyo ni mkosi kwani kunaashiria ukame katika eneo lao hivyo ili kuepukana na jambo hilo njia pekee ya kuzuia ni kumuua mnyama huyo. AWF inabainisha mikakati ya kulinda mnyama huyo na kuhakikisha uendelevu wa kizazi chake kwa kushirikisha jamii na kukuza uelewa kwa umma.
WWF na washirika wake wanafanya kampeni mbalimbali kuwaelimisha watumiaji wa bidhaa za wanyamapori kuacha imani za kishirikina na kuacha kuua mnyama huyo. Aidha, inafanya kazi na jamii zinazoishi karibu na maeneo ambayo wanyama hao wanapatikana kwa kuwapa mbinu mbadala za kiuchumi ikiwemo kilimo endelevu kinachowafanya waache kuwinda wanyama hao walio hatarini ili kupata chakula.
Kwa Tanzania, Mradi wa Uhifadhi wa Kakakuona Tanzania (TRCO) unaweka mikakati na mipango mbalimbali ya kuokoa kizazi cha kakakuona na kukifanya kiwe endelevu.
Katika kutekeleza miradi ya uhifadhi wa kakauona TRCO kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa kufanya tafiti mbalimbali juu ya utambuzi wa kakakuona, imani ya jamii kuhusu mnyama huyo, kuenea kwake na biashara dhidi ya mnyama huyo.
Juhudi hizo za TRCO na wadau wengine zinaweza kuzaa matunda kuhakikisha uendelevu wa kizazi cha kakakuona ikiwa jamii itaelimishwa juu mnyama huyo asiye uhusiano wowote na imani za kijadi wala ushirikina.