Tarura Karagwe yajikita barabara za lami

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Karagwe imejikita kuongeza mtandao wa barabara za lami kutoka kilometa 25.29 hadi kilometa 28.29 ifikapo Novemba mwaka huu mara baada ya kukamilika kwa mradi wa barabara ya Nyakahanga-Nyabionza Masheli kilometa tatu za lami.

Mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025 zimeweka Jiwe la Msingi katika barabara hiyo ambayo mradi wake umefikia asilimia 83.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Karagwe, Kalembula Malimi amesema kuwa serikali iliidhinisha Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo kwa kiwango cha lami na mpaka sasa mkandarasi amelipwa Sh bilioni 1.1. Amesema barabara hiyo inachochea uchumi wa wananchi na kurahisisha huduma za jamii.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi amewataka wananchi kutumia fursa za uwepo wa barabara kufanya biashara kwa nyakati zote ili kukuza uchumi wao na kuchangia Pato la Taifa,kupeleka watoto shule na kuinua familia zao.
Amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini kwani ndiko kwa wananchi wanaotegemea kusafirisha mazao kwa ajili ya kujipatia kipato na kuendesha familia zao kupitia barabara bora na imara.

Kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Karagwe kwa asilimia 78 barabara zake zinapitia muda wote huku asilimia 22 barabara zikiwa katika matengenezo na ukarabati wa mara kwa mara.



