Ngajilo ahaidi kuwa sauti ya wananchi Iringa Mjini

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, ameahidi kuwa sauti ya wananchi katika raha na shida, akisisitiza kuwa maendeleo ya Iringa hayataachwa kwa maneno bali vitendo.
“Iringa tunatamani kutoka hapa tulipo kwenda juu zaidi, tunahitaji kuukuza mji wetu kwa huduma, biashara na maendeleo kwa ujumla. Tunatamani kuwa jiji,” alisema wakati Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Stephen Wasira akizindua rasmi kampeni za ubunge na udiwani jimbo la Iringa Mjini.
Alimshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza miradi ya barabara inayounganisha kata mbalimbali.

Aliahidi kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Rais Samia kuunganisha mitaa yote, akiweka wazi kuwa Iringa ina fursa kubwa za kiuchumi zinazohitaji kuendelezwa kwa ubunifu na mshikamano wa wananchi.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, aliyetumia mkutano huo kuzungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali, akisema maendeleo makubwa yaliyofikiwa hayahitaji kura za huruma bali ni uthibitisho wa uongozi thabiti wa Rais Dk Samia.
“Hapa jimbo la Iringa Mjini kwa miaka mitano tumefanikisha ujenzi wa shule mpya nne na madarasa 114 bila wananchi kuchangia,” alisema.

Alisema sekondari nne mpya zimejengwa zikiwa na madarasa 134 na katika afya, wamejinge zahanati tatu, vituo vya afya vitatu na kuboresha hospitali,” alisema.
Alisema mji wa Iringa ulikuwa hauna maji, sasa una maji ya uhakika.
Alibainisha pia mpango wa kujenga shule mpya za msingi na sekondari 22 pamoja na zahanati saba, akihimiza wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi hususan ufugaji.
“Hii ni fursa kubwa kwa wananchi wa Iringa. Ufugaji una soko la uhakika katika kiwanda cha Asas cha kusindika maziwa,” alisema.
Alisema CCM katika Ilani yake imehimiza uanzishwaji wa viwanda vipya kama moja ya hatua ya kuongeza thamani ya malighafi zinazozalishwa nchini na kuongeza ajira.
Wasira pia alitaja miradi mikubwa ya kimkakati kama reli ya kisasa (SGR) na upanuzi wa umeme kuwa imesaidia kuimarisha uchumi na kuongeza ajira, akihitimisha kwa msisitizo:
“Hatuombi kura za huruma kwa Rais Samia. Tunaomba kura kwa sababu ameweza na bado anaweza kuendeleza mapinduzi ya maendeleo.



