Austria yafadhili miradi ya umeme Tanzania

VIENNA : SERIKALI ya Austria kupitia Benki ya UniCredit imeahidi kuipatia fedha Serikali ya Tanzania Euro milioni 20 sawa na Sh bilioni 60 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia jua na takataka.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Merl Solar Technologies GmbH, Hannes Merl alipofanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba juzi pembeni ya Mkutano Mkuu wa 69 wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic unaoendela jijini Vienna, Austria.
Ili kuanza utekelezaji wa miradi hiyo, Mramba ameikaribisha kampuni hiyo nchi ni ili kukutana na wataalamu na kuanza kufanya maandilizi stahiki ya miradi hiyo mipya ya kuzalisha umeme huku akiahidi kutoa ushirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo.
Mramba ameeleza kuwa Kampuni ya Merl imeshatekeleza miradi mbalimbali ya umeme wa jua nchini akisema: “Kampuni hii imetekeleza miradi ya umeme katika vijiji 10 katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2017”. SOMA: Tanesco yajizatiti huduma ya umeme Mtwara, Lindi
Ametaja miradi hiyo ni ya kontena 14 za kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua katika Wilaya za Kongwa mkoani Dodoma, Mlele mkoani Katavi, pamoja na Uyui mkoani Tabora ambapo mradi huo uligharimu Sh bilioni 16.2. Ameongeza kuwa miradi hiyo imewezesha kuzipatia umeme nyumba na makazi 812, nyumba za ibada 27, shule sita na vituo vya afya vinane.
Mramba ameishukuru Serikali ya Austria kwa kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi pamoja na nia ya kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa Mkakati Mahususi wa Nishati unaolenga kupeleka umeme kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2030