Wadau waongeze kasi elimu ya mpigakura

LEO imetimia siku 30 tangu kampeni za vyama vya siasa zizinduliwe nchini Tanzania. Kampeni hizi zimekuwa fursa muhimu kwa vyama vyote vyenye nia ya kuwania madaraka kutangaza sera zao, ilani za uchaguzi na mipango wanayoahidi kuitekeleza, iwapo wananchi watawapa ridhaa Tunaendelea kupongeza wananchi, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, kutokana na kampeni kuendelea kufanyika katika hali ya utulivu na amani.
Wananchi wanaendelea kupata nafasi ya kusikiliza na kutathmini viongozi na vyama kupitia majukwaa tofauti ya kampeni, huku hali ya usalama ikiwa imetawala. Ikiwa zimebaki siku 33 kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, wananchi bado wana nafasi ya kuendelea kuwasikiliza wagombea wa udiwani, ubunge, uwakilishi na uwaziri kwa ajili ya kufanya uchaguzi sahihi.
Tunapongeza mamlaka zinazohusiana na uchaguzi, zikiongozwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo imesimama kidete kuhakikisha mchakato huu wa demokrasia unafanikiwa, huku ikiendelea kuratibu utoaji wa elimu ya mpigakura.Mamlaka ya tume katika kutoa elimu hiyo nchi nzima, yanatokana na Kifungu cha 10 (1) (g) na (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Na. 2 ya Mwaka 2024. Inafanya kazi ya kuratibu na kusimamia taasisi, asasi na watu wanaotoa elimu hiyo ambao wamepata kibali.
Elimu hii hutolewa kwa wananchi wote, kwa lengo la kuwawezesha kuelewa kuhusu sheria, kanuni, taratibu za mchakato mzima wa uchaguzi, wajibu wao na umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi. Vilevile, ni elimu isiyokuwa na hisia, ubaguzi wala itikadi za kisiasa, kidini au kikabila. Sambamba na elimu, pia wapigakura wanapata taarifa ambayo inajibu maswali ya msingi kama vile, wapi atapigia kura, lini, muda gani, atarajie nini akifika kituoni na namna atakavyopata matokeo ya uchaguzi.
Kwa hiyo, elimu na taarifa hizi ni muhimu zinapowafikia wadau na wapigakura kwa usahihi na kwa wakati, kwani zinawafanya wajiamini na hivyo kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.Kama ilivyoainishwa na INEC, elimu ya mpigakura inamwezesha mwananchi kuwafahamu wagombea, kujua sifa za kuwa mpigakura, kujua wapi, lini na muda wa kupiga kura, kujua taratibu zinazotakiwa kufuatwa, awapo katika kituo cha kupiga kura.
Elimu hii ikitolewa ipasavyo, itapunguza au kuondoa kabisa matukio ya kura kuharibika, kwani upo uwezekano mkubwa wa baadhi ya watu kukosea namna ya kupiga kura, si kwa makusudi bali kwa sababu ya kutofahamu mambo ya msingi ya upigaji kura. Vilevile, wapo ambao huamua kubaki nyumbani kwa sababu tu ya kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu mchakato wa uchaguzi, ikiwemo kujua wapi na lini watapiga kura.
Wadau walioidhinishwa kufanya kazi hiyo ya kutoa elimu kwa mpigakura, ni kuendelea na kasi kwa njia sahihi zilizowekwa na tume, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata elimu hiyo kabla ya Oktoba 29, hatimaye ashiriki ipasavyo kuchagua kiongozi anayemtaka.