Wawakilishi wetu wa kimataifa tupambane

TIMU nne za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya kimataifa za Yanga, Simba, Azam FC na Singida Black Stars zimeanza vizuri mashindano hayo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Timu hizo zote zilicheza mechi zake hizo za kwanza ugenini na kuanza vizuri kwa ushindi wa mabao tofauti, huku Yanga wakishinda mabao 3-0 ambapo walicheza dhidi ya Timu ya Angola ya Wilete na Simba ilishinda 1-0 dhidi ya Gaborone United nchini Botswana. Wote walicheza mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Azam FC yenyewe ilicheza dhidi ya El Merriekh Bentui ya Sudan Kusini na Singida BS ilicheza dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda na kushinda mabao 2-0. Timu hizo zote mbilli zilicheza mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.

Tunawapongeza wawakilishi wote hao wa Tanzania katika mashindano hayo ya Kimataifa na Singida BS ikishiriki kwa mara ya kwanza kabisa, wakati Azam ikishiriki mara nyingi.

Timu hizo zinacheza mechi za marudiano mwishoni mwa wiki hii na kama zikipata ushindi wa jumla, basi zitacheza raundi inayofuata na hivyo kuendelea kuchanja mbuga na kuiongezea nchi pointi ili iendelee kuingiza timu nne katika michuano ya CAF.

Ni matumaini yetu kuwa timu hizo zote zitafuzu kwa raundi inayofuata katika mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Tunawaombea dua wawakilishi wetu hao kwa kucheza mashindano hayo ya Afrika na kuwataka wapambane ‘kiume’ ili kuhakikisha wanashinda michezo yao, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea hatua inayofuata.

Simba kwa muda mrefu imekuwa ikifanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika na kufika hatua ya robo fainali mara nyingi lakini hilo lisiwe sababu ya kubweteka na kujisahau kuwa michuano hiyo ni migumu.

Msimu uliopita, Simba ilijikuta ikicheza Kombe la Shirikisho baada ya kumaliza ya tatu katika Ligi Kuu Tanzania Bara, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Azam FC iliyotolewa na wawakilishi wa Rwanda, baada ya kufungwa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini hiyo isiwatie jeuri kwamba msimu huu watafika mbali kama kawaida yao.

Yanga kabla ya Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho, ilihamishiwa huko baada ya kuanza katika Ligi ya Mabingwa na kutolewa, mfumo ambao sasa haupo baada ya CAF kuufutilia mbali, hivyo timu za Ligi ya Mabingwa hazipati nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho kama zamani.

Wawakilishi wetu wote wa Kombe la Mabingwa na wale wa Shirikisho wagangamale ili kushinda mechi zao, kwani sasa hata ukifika raundi gani na kutolewa, huwezi kupelekwa Kombe la Shirikisho kama zamani.

Ukitolewa umetoka tu, hakuna kuhamishiwa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya CAF kubadili mfumo huo kama Afrika. Wawakilishi wetu wapambane ili wavuke raundi hii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button