2030 Tanzania yote itawaka umeme

ARUSHA: Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi( CCM) Dk Samia Suluhu Hassan amewaahidi wananchi mkoani Arusha kuwa kufikia mwaka 2030 maeneo yote ya nchi yatakuwa yamefikiwa na huduma ya umeme.
Akizungumza Oktoba 01, wakati akihutubia wananchi wa Arumeru mkoani Arusha ikiwa ni muendelezo wa kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, Dk Samia amesema kasi waliyonayo katika kutoa huduma za umeme inawapa imani ya kufikia lengo hilo.
” Kwenye umeme ndugu zangu tunakwenda kumaliza vitongoji vilivyobaki, ilani ilitutaka tupeleleke vijiji vyote tulimaliza vijiji tukajiongeza tunakaanza na vitongoji na tunavyozungumza nusu ya vitongoji vya Tanzania tayari vina umeme amesema Dk Samia na kuongeza
“Miaka inayokuja tunamaliza umeme kwenye vitongoji vyote tukifika 2030 Tanzania yote inawaka umeme” amesema Dk Samia.
Katika hatua nyingine Dk Samia amesema ikiwa CCM itapewa ridhaa ya kuongoza dola kwa mara nyingine Serikali itaendelea na agenda yake ya nishati safi ya kupikia ili kuwanusuru wakina mama na maradhi yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa.