Mabasi 90 yahudumia njia ya Kimara-Kivukoni

SERIKALI imesema imeamua kuingiza mabasi 60 mapya kwenye Barabara ya mabasi yaendayo haraka njia ya Kimara hadi Kivukoni mkoani Dar es Salaam.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema njia hiyo ilikuwa na mabasi 30 yanayofanya kazi, hivyo sasa njia hiyo itakuwa na mabasi 90.

Majaliwa amesema hayo alipofanya ziara kukagua hali ya utoaji huduma ya usafiri kwa mabasi yaendayo haraka kwa njia ya Kivukoni hadi Kimara.

SOMA: Maagizo ya Waziri Mkuu ukamilishaji miundombinu mwendokasi yazingatiwe

“Serikali yenu baada ya kuruhusu makampuni binafsi, tumeona tuchukue mabasi 60 kutoka Kampuni ya Mofat yaingie katika barabara hii na yameanza kutoa huduma leo. Malengo yetu ni kuondoa kadhia ya usafiri kwenye njia hii” amesema.

Ameongeza: “Yatajumulishwa na haya 30 yaliyokuwa yakitoa huduma awali na leo mabasi mapya yameanza kutoa huduma na yatakuwa yanatumia umeme na gesi. Natoa wito kwa makampuni mbalimbali kujitokeza na kujenga vituo vya gesi.”

Majaliwa ameiagiza kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART) na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) wasimamie matumizi ya kadi za kielektroniki katika utozaji wa nauli, badala ya kutumia fedha taslimu ili kudhibiti upotevu wa mapato.

“Na tumeagiza kadi hizi zisiwe za mabasi haya peke yake, tunataka zitumike kwenye viwanja vya mipira, usafiri wa Azam marine, SGR (Reli ya Kisasa), vituo vya mabasi. Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry Silaa, tunataka hili likamilike kwa haraka” amesema.

Ameongeza: “Waziri mwenye dhamana kwenye suala la teknolojia, hakikisha suala hili linakamilika kwa wakati na kadi hizi zitakapotoka, hakikisha zimeunganishwa na mifumo yote ili kadi moja mtu aweze kuitumia katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kusafiri, kuangalia mpira na kufanya manunuzi.”

Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na DART wasimamie usafiri huo, ili kupunguza kero ya usafiri wa mabasi hayo.

Majaliwa aliwataka wananchi kufuata utaratibu uliowekwa ili kuondoa hali ya kugombania magari, iliyosababisha uharibifu wa miundombinu hapo awali.

“Serikali imeamua kuruhusu sekta binafsi kushiriki kwenye biashara ya usafiri wa mwendokasi. Tayari makampuni manne yamesaini mikataba na kuanza kuagiza mabasi. Kampuni ya Mofat peke yake imekwishaingiza mabasi 150 kwa ajili ya njia za katikati ya jiji na Mbagala,” amesema.

Majaliwa amesema mabasi mapya yamegawanywa kwenye njia tofauti, ikiwemo ya Kivukoni–Kimara, katikati ya jiji–Mbagala, Mbagala Rangi Tatu kupitia Kigamboni na Gongo la Mboto.

Amesema serikali imetangaza zabuni kwa kampuni binafsi kuwekeza katika vituo vya kuchaji magari ya umeme
na gesi na kituo cha kwanza cha gesi kipo hatua za mwisho za ukamilishaji.

Majaliwa amesema serikali inaendelea pia na ujenzi wa barabara za mwendoksasi za Morocco–Mwenge–Tegeta na Ubungo–Buguruni kuelekea Kiwanja cha Ndege cha cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ili kupunguza msongamano.

Chalamila amesema kuongezwa kwa mabasi mapya ya mwendokasi kumetoa suluhisho la changamoto za usafiri Dar es Salaam na akaahidi miundombinu italindwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button