Samia ataja mikakati ya utalii Arusha

ARUSHA : MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ametaja mikakati ya kukuza utalii Arusha. Miongoni mwa mikakati hiyo ni ukarabati kiwanja cha ndege kilichopo Kisongo, ujenzi wa kituo cha mikutano na mji maalumu wa michezo kwa ajili ya michuano ya fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON).

Alitaja mikakati hiyo kwenye mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana. Samia alisema mambo mengi yamefanyika kukuza utalii katika miaka mitano iliyopita, ikiwa ni pamoja na kupokea watalii milioni tano ndani na nje ya nchi.

Alisema lengo la serikali yake, kama ilivyoagiza ilani ya uchaguzi ya chama chake ni kufikisha watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030. Samia alisema Kiwanja cha Ndege cha Arusha kimeboreshwa kwa gharama ya Sh bilioni 17 na kuanzia Januari mwakani kitatumika usiku na mchana, hivyo kusaidia safari za watalii, wafanyabiashara, wana Arusha na Watanzania kwa ujumla.

“Kingine ni Kiwanja cha Ziwa Manyara Karatu, pale tumetumia Sh bilioni 88.5 kuweka meta 1,500 za lami lakini pia jengo la abiria litakalobeba abiria 150 na eneo la maegesho ya magari litakalokuwa na uwezo wa magari 67 pia tutaweka lami barabara inayoingia ndani ya Kiwanja cha Ndege cha Karatu, katika hatua nyingine ya kukuza utalii,” alisema.

Samia alisema chama chake kitakapopata ridhaa ya kuongoza tena, kitaongeza ndege nyingine nane za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ili shirika hilo lijitanue kwenda maeneo mbalimbali na kukuza biashara na utalii. “Tumeimarisha sana shirika la ndege katika kipindi chetu cha miaka mitano, tumeongeza ndege nane na kipindi kijacho tutaongeza tena,” alisema.

Pia, Samia alisema utatumika utalii wa michezo na umejengwa uwanja kwa ajili ya mashindano ya Afcon. “Lakini uwanja ule pia unakwenda kuwa kivutio cha watalii, kwa sababu pale ulipo tutajenga kituo kinaitwa Mji wa Afcon. Niwaambie kwamba, uwanja ule tuumeshaukamilisha kwa asilimia 63 na utakapokamilika utabeba watu 32,000 na mpaka Julai mwakani uwanja utakuwa umekamilika, tutaendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa Kijiji cha Afcon,” alisema.

Tanzania, Kenya na Uganda zinatarajiwa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa kwa timu za taifa Afrika mwaka 2027. Kuhusu kujenga kituo kipya kikubwa cha mikutano cha kimataifa, Samia alisema wanakusudia kujenga kituo hicho kikiwa na hoteli kubwa kubwa na fursa zote za mikutano. “Lakini kule Ngorongoro Lengai tunakwenda kujenga vizuri sana kituo cha urithi wa kijiolojia kwa watalii watakaopenda kuwa na mambo ya kihistoria, mambo ya kisayansi yanayoendana na hayo,” alisema.

Aliongeza: “Lakini pia katika kukuza utalii huo, lazima tukuze na makazi na mahoteli. Kwa hiyo, tunakwenda kuvutia wawekezaji wakubwa wajenge mahoteli ya nyota kubwa, ili watalii waje kwa wingi wakiwa na uhakika wana sehemu nzuri za kufikia.”

Samia alisema Ukanda wa Kaskazini kuanzia Tanga mpaka Arusha na kufika mpaka Musoma watajenga reli ya kisasa (SGR), ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu. Alisema miongoni mwa vipaumbele vyao katika miaka mitano ijayo, ni kuendeleza kongani za viwanda wakiwa na mpango wa kuendeleza na kufufua viwanda ambavyo havizalishi vizalishe na waweke vingine kwenye wilaya, vitakavyofanya kazi ya kuongeza thamani mazao yanayopatikana kwenye wilaya.

“Na kwa hilo katika Mkoa wa Arusha tunakwenda kujenga kiwanda cha magadisoda kitakachokuwa Monduli na tayari mambo yanayohitajika yapo tayari, tunasubiri kijengwe. Kwa hiyo, ajira zitakwenda kuwa nyingi kwa vijana huko,” alisema Samia. SOMA: Manyara yapamba moto mapokezi ya Dk Samia

Kuhusu barabara, Samia alisema watakamilisha miradi yote inayoendelea kwa sasa na mipya iliyokuwa kwenye ilani, watazijenga huku akijivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya kwenye mkoa huo pamoja na kufanya uwekezaji mkubwa kwenye mambo ya kijamii na kusisitiza kuendelea kujenga miundombinu ya elimu.

Alisema, “Hata wale watu wenye uhitaji maalumu, serikali imejipanga vizuri sana kama maelekezo ya kimataifa yanavyosema, asiachwe mtu nyuma na sisi Tanzania hatutaki kuacha mtu nyuma.” Kuhusu Kituo cha Mabasi cha Arusha, Samia alisema kimeshaanza kujengwa kikitumia takriban Sh bilioni 14.3 lakini pia wakitarajia kujenga soko kubwa la wamachinga.

Alisema, “Pia tutaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wafanyabiashara, ambayo imewainua wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.” Pia, Samia alisema madini yametumika kuimarisha uwezo wa nchi kujitegemea kiuchumi. “Tumeanza kuweka akiba yetu ya dhahabu ndani ya benki kuu na akiba ile imekuwa ikikua mwezi hadi mwezi na ndio maana Shilingi yetu nayo inakua madhubuti kwenye uchumi wa dunia,” alisema.

Pia, Samia alizungumzia mashamba matano ya Kiliflora Arusha na kusema wameafikiana, mwekezaji ameshindwa kuendelea nayo. Alisema serikali yake inaangalia uwezekano wa kuyawekea miundombinu na kutumia kwenye Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT). “Kwa ujumla, CCM serikali zake za awamu zote tumeweza na mkiturudisha tena tunaweza… tuna kila njia, mbinu na fursa ya kuitumia tuweze kutekeleza yale tuliyoyaweka kwenye ilani,”alisema Samia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button