Mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya mama wa kambo
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mkazi wa Masoko wilyani Rungwe, Tatizo Mzumbwe kwa tuhuma za mauaji ya mama yake wa kambo aliyekuwa albino.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Benjamin Kuzaga imemtaja mama huyo kuwa ni Merry Yohana (61) na ameuawa kwa kukatwa panga kichwani.
Amesema tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Mapinduzi kilichopo Kata ya Masoko, Tarafa ya Isangati.
SOMA: Matawi sita ufufuo na uzima yafungiwa Mbeya
Kamanda Kuzaga amesema kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza msako mkali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa majira ya usiku huko Kijiji cha Mapinduzi.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia kuhusu mashamba ambapo mtuhumiwa alikuwa akimshinikiza mama huyo wa kambo kugawa mashamba ya urithi yaliyoachwa baada ya baba yake kufariki.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa baadhi ya vijana kuacha tamaa ya kutaka kujipatia mali kwa njia zilizo kinyume na sheria. Uchunguzi unakamilishwa ili hatua nyingine zichukuliwe dhidi ya mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria.” amesema Kamanda Kuzaga.



