Mabadiliko tabianchi yaleta changamoto kilimo

WAKULIMA mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro na Manyara wanakumbwa na changamoto kubwa ya kuendeleza kilimo kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan ukame wa mara kwa mara, mvua zisizo na utaratibu na kuongezeka kwa joto.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanyika nchini, hali hiyo imeendelea kudhoofisha uzalishaji wa mazao na kuathiri maendeleo ya sekta ya kilimo, ambayo ndiyo mhimili wa uchumi wa taifa. Ripoti ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) inaonesha kuwa sekta ya kilimo inachangia asilimia 29 ya Pato la Taifa (GDP) na inahusisha zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanaoishi vijijini. “Mwendo wa mvua bila utaratibu, au ukame wa mara kwa mara, unachochea kuporomoka kwa tija ya mazao,” ripoti imeeleza hivyo.

Katika Mkoa wa Dodoma, utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wakulima wanatambua uwepo wa mabadiliko ya tabianchi, lakini wengi hawana uwezo wa kubadili mbinu zao za kilimo. “Wengi wanajua tatizo, lakini hawana rasilimali za kutumia mbegu za ukame au mifumo ya umwagiliaji wa kisasa,” ripoti imeeleza.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), mikoa ya kaskazini pia imeanza kushuhudia ongezeko la joto la kati ya nyuzi 0.5 hadi 1.2 za sentigredi, hali ambayo imeathiri ustawi wa mazao kama mahindi, mpunga na maharage.

“Mimi sina matumaini tena,” anasema mkazi wa Makuyuni, Manyara, aliyekosa mavuno ya mahindi msimu uliopita. “Muda wote wa kiangazi nimeharibu mazao yangu, sasa njaa inakaribia katika kaya yangu,” anaongeza. Serikali kupitia mpango wake wa NDC imetambua hali hiyo kama changamoto kuu kwa maendeleo ya taifa.

Hata hivyo, utekelezaji wa mipango ya kukabiliana na hali hiyo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa bajeti, ukosefu wa ufadhili wa kimataifa na miundombinu duni ya umwagiliaji. Tafiti zinaonyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yameongeza ukame na mafuriko ambayo huharibu mashamba, kubomoa miundombinu ya kilimo na kusababisha mmomonyoko wa udongo.

Misimu ya mvua pia imekuwa ikibadilika, wakati mwingine ikiwahi na wakati mwingine ikichelewa kuanza, hali inayosababisha kupungua kwa kipindi cha ukuaji wa mazao kama mahindi, mpunga na mtama. Ripoti za watafiti zinaonesha kuwa ongezeko la joto kwa nyuzi mbili za sentigredi linaweza kupunguza mavuno ya mahindi kwa zaidi ya asilimia 13 kufikia mwaka 2050, jambo linalotia wasiwasi kwa usalama wa chakula wa taifa.

Aidha, kuongezeka kwa joto na mabadiliko ya mvua kumechangia kuenea kwa magonjwa ya mimea na mashambulizi ya wadudu, huku ukame unaorudiwa na uhaba wa maji vikileta shinikizo kubwa kwa rasilimali za maji. Hali hii si tu kwamba inahatarisha kilimo cha umwagiliaji, bali pia inaathiri uzalishaji wa umeme na maisha ya watu vijijini wanaotegemea kilimo kama chanzo kikuu cha kipato.

Wataalamu wa mazingira na kilimo wameonya kuwa bila uwekezaji wa kutosha katika teknolojia, elimu kwa wakulima na huduma za ugani, hali hii inaweza kuongeza umaskini na migogoro kati ya wakulima na wafugaji kutokana na upungufu wa ardhi na malisho. Wanasema kuwa ili Tanzania iweze kukabiliana na changamoto hizo, ni lazima ichukue hatua madhubuti kubadilisha mfumo wa uzalishaji wa kilimo na kuongeza uwezo wa wakulima wadogo kujitegemea.

 

Hatua muhimu ni kuimarisha kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi (climate-smart agriculture), kinachojumuisha matumizi ya mbegu za ukame, mazao yanayokomaa mapema na teknolojia za umwagiliaji wa kisasa kama drip irrigation na sprinkler systems. Kwa mujibu wa TMA na mpango wa NDC (2021), uwekezaji katika kilimo kinachotumia maji kwa ufanisi unaweza kuongeza tija ya mazao kwa zaidi ya asilimia 20 katika maeneo kame.

Serikali pia inahimizwa kuimarisha huduma za ugani na elimu kwa wakulima kwani tafiti zimeonesha kuwa wengi wanatambua tatizo, lakini wachache wanajua mbinu sahihi za kukabiliana nalo. Kupitia mafunzo endelevu, redio za kijamii na vituo vya elimu vya wakulima, taarifa na maarifa ya tabianchi yanaweza kusambazwa kwa upana zaidi vijijini.

Wataalamu wanashauri pia kuimarishwa kwa miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi wa maji kwa kujenga mabwawa madogo, kuvuna maji ya mvua na kutumia visima vidogo ili kuwezesha uzalishaji wa mazao hata wakati wa ukame. SOMA: Kilimo himilivu; suluhu mabadiliko ya tabianchi

Vyuo na taasisi za utafiti kama Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) vinatakiwa kupewa kipaumbele katika utafiti wa mbegu na teknolojia zinazoweza kustahimili joto, magonjwa na upungufu wa maji. Ripoti ya IPCC (2022) inaeleza kuwa utafiti wa ndani na ubunifu wa kiteknolojia ni silaha muhimu kwa nchi za Afrika kujenga ustahimilivu wa kilimo.

Hata hivyo, utekelezaji wa miradi hiyo unahitaji fedha, hivyo serikali inapaswa kutenga bajeti maalum kwa ajili ya miradi ya tabianchi sambamba na kuvutia ufadhili wa kimataifa kupitia Green Climate Fund (GCF) na Adaptation Fund, kama ilivyoainishwa kwenye mpango wa NDC (2021).

Wataalamu pia wamesisitiza umuhimu wa kujenga ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji, hasa katika matumizi ya ardhi na vyanzo vya maji, ili kupunguza migogoro inayotokana na upungufu wa rasilimali hizo. Aidha, ni muhimu kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa za hali ya hewa kupitia simu, redio na majukwaa ya kidijitali ili wakulima wapate taarifa mapema na kupanga shughuli zao ipasavyo.

Kwa mujibu wa TMA (2023), upatikanaji wa taarifa kwa wakati ni nyenzo muhimu ya kuongeza tija na kupunguza hasara za mazao. Wataalamu wanasema kuwa hatua hizo zikitekelezwa ipasavyo, Tanzania itaweza kulinda sekta ya kilimo, kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umaskini katika jamii za vijijini.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→ http://Www.Payathome9.Com

  2. Google pays $220 an hour online. My close relative had been unemployed for nine months, but last month, she received a $25k paycheck by working from home for 10 hours a day. Everyone should try this job now—just use this link. COPY THIS →→→→ https://Www.Salary7.Zone

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button