Sirro ahimiza masomo ya sayansi sekondari

KIGOMA: Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amewataka wazazi mkoani Kigoma kuhamasisha watoto wao kuyapenda masomo ya sayansi ili kuzalisha idadi kubwa ya wataalamu.
Balozi Sirro ametoa amesema hayo wakati akikagua ujenzi wa maabara tatu za masomo ya kemia, baiolojia na fizikia katika Shule ya Sekondari ya Kakonko mkoani Kigoma ukiwa ni moja ya miradi inayotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania(TEA) kwa gharama ya Sh milioni 180.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa serikali imekuwa ikihimiza wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaofanya vizuri ili kusaidia kuongeza morali ya kuinua wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na kupata idadi kubwa ya wataalam wanaotokana na kozi mbalimbali zinazotokana na masomo ya sayansi.
Amesema kuwa wazazi wana jukumu kubwa kuwahimiza na kuwaandaa watoto wao kusoma masomo yao sayansi sambamba na kuwasaidia katika kuwawekea mazingira mazuri ambayo watoto watasoma masomo hayo na kuyapenda.
Akizungumzia ujenzi wa maabara hizo Mkuu huyo wa mkoa Kigoma amewataka wanafunzi, wazazi na jumuia nzima ya shule hiyo kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo muhimu ya kujifunzia na kufundishia ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kunufaisha kundi kubwa la watanzania.

Awali Mkuu wa Shule hiyo, Anatoria Paul alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeongeza hamasa kwa wanafunzi wengi kusoma masomo ya Sayansi sambamba na kufanya vizuri katika masomo hayo kutokana na kuwepo kwa vifaa kutosha vya kujifunzia na kufundishia.



