Halotel waeleza walivyowafikia wateja

KAMPUNI ya Mawasiliano ya Halotel imesema hadi kufikia Septemba mwaka huu imefanikiwa kufikia wateja milioni 16.5 kupitia huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo.

Akizungumza leo Oktoba 16,2025 katika maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo nchini Tanzania, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara Halotel, Abdallah Salum amesema katika kuunganisha wananchi, Halotel itaendelea kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya mawasiliano yenye ubora, gharama nafuu na mahali popote.

“Mafanikio haya yametokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya mawasiliano, na ndiyo maana tunahudumia mamilioni ya wateja kwa kuwaunganisha kutoka vijijini hadi mijini, hasa maeneo ambayo hapo awali hayakuwa na mtandao,” amesema Salum.

Naye Mkurugenzi wa Halotel nchini, Bui Van Thang amesema kwa kipindi cha miaka 10 wamekuwa sehemu ya maisha ya watanzania kwa kutoa huduma zenye ubunifu na kuhakikisha kila mmoja anabaki kuunganishwa na dunia.

“Tunajivunia mchango wetu katika kukuza uchumi wa watanzania kidijiti na kutoa fursa za maendeleo kwa wananchi wote. Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu ya tunaenda mbele pamoja, ikionyesha dhamira ya Halotel kuendelea kuboresha huduma zake, kuleta ubunifu mpya na kushirikiana na wateja katika safari ya ukuaji wa teknolojia nchini,” amesema.

Ameongeza kuwa kupitia maadhimisho hayo wamezindua promosheni maalumu kwa wateja kuweza kujishindia zawadi ya gari aina ya Subaru Forester kupitia miamala ya Halopesa.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Halotel, Roxana Kadio amesema kampuni hiyo inaendelea kuimarisha sifa yake kama chapa inayojali wateja kwa kutoa si tu huduma bora za mawasiliano, bali pia uzoefu unaoboresha maisha ya watumiaji wake, hivyo jamii itumie huduma hiyo kwani ni rahisi.

“Kampuni yetu itaendelea kushirikiana na serikali, jamii na wateja wake katika kuimarisha huduma za mawasiliano, kuchochea maendeleo ya kidijiti na kuinua maisha ya watanzania,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button