Mwinyi : Mabasi ya Umeme Kuleta Mapinduzi

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais anayeongoza, Dk Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuanzishwa kwa mabasi ya umeme kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri wa umma na kupunguza uchafuzi wa mazingira katika jiji la Zanzibar.
Akizungumza na wafanyabiashara katika eneo la soko la Darajani, ambapo alitembelea maeneo mbalimbali na pia kuwalisha ndege Njiwa katika eneo hilo, Dk. Mwinyi alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa mageuzi katika sekta ya usafiri baada ya kuzinduliwa kwa huduma za teksi za baharini, ambazo sasa zinawaunganisha wakazi wa visiwa mbalimbali.
“Baada ya kuzindua teksi za baharini, hatua inayofuata ni kuleta mabasi ya umeme. Tukiahidi, tunatekeleza,” alisema Dk. Mwinyi huku akishangiliwa na wafanyabiashara. SOMA: Ngajilo aahidi kushughulikia kero ya barabara na mfereji Isakalilo
Alisema mabasi hayo yatasaidia kupunguza mitetemo na moshi wa magari yanayotumia mafuta, ambayo yamekuwa tishio kwa majengo ya kihistoria ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, urithi wa dunia uliosajiliwa na UNESCO.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya eneo la Darajani baada ya ukarabati mkubwa, akisema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya biashara na mandhari ya mji ili iwe safi, yenye mpangilio na kuvutia watalii. “Mji wa Zanzibar lazima uwe wa kisasa, wenye mazingira rafiki kwa biashara na utalii,” alisema.
Alibainisha pia mipango ya kujenga kituo kipya cha maegesho Malindi, kupanua barabara ya Malindi–Mnazimmoja kuwa ya njia nne, na kutekeleza mradi wa BIG Z utakaowezesha ujenzi wa maduka ya kisasa kutoka Kariakoo hadi Kisiwandui. Vilevile, aliagiza ZECO kuweka transformer mpya Darajani ili kutatua changamoto za umeme zinazokwamisha biashara.
Dk. Mwinyi aliahidi pia kuongeza mfuko wa mikopo isiyo na riba kwa wafanyabiashara wadogo na kupitia upya mfumo wa kodi kwa ushauriano na uongozi wa CCM, akisisitiza umuhimu wa amani wakati wa uchaguzi. “Katika uchaguzi wa Oktoba 29, nendeni mkapige kura mapema kisha mrejee kazini; amani itakuwepo. Tukiipenda amani na maendeleo, tumpigie kura CCM,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed, alimuelezea Dk. Mwinyi kama kiongozi mwenye nidhamu na anayetekeleza ahadi zake.
Wafanyabiashara wa Darajani, wakiongozwa na Bi. Iptsam Mohamed Rashid, walimshukuru Rais kwa kubadilisha sura ya soko hilo, kutoka vibanda 44 vya muda hadi zaidi ya maduka 540 ya kudumu, pamoja na kurejesha bustani, kituo cha mabasi na maegesho.