Watanzania tusimamie misingi, utu wema kulinda amani ya nchi

AMANI ya Tanzania imejengwa katika misingi ya utu, uzalendo, mila na tamaduni njema zinazomjenga kila mwananchi kuona ni tunu ya kipekee kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Historia inaonesha tangu kuasisiwa kwa Taifa la Tanzania, misingi ya amani imechangia kulikuza na kufikia leo ambapo Watanzania na dunia inashuhudia kupokezana vijiti vya utawala kufikia awamu sita kwa amani na utulivu mkubwa.
Katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025, kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda tunu ya amani kwa kusimamia misingi ya utu, uzalendo na matashi mema.
Tunashauri kila Mtanzania kuwa na kiu ya kuona nchi yake inaendelea kuwa na amani ili ahadi, sera na mipango iliyowekwa kabla na itakayotekelezwa baada ya uchaguzi iweze kutekelezeka.
Ni wazi Watanzania wamesikia au kushuhudia machafuko, vita na vurugu katika mataifa mbalimbali duniani, hali inayochangia kuharibu mali na kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.
Penye vita hakuna shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanyika, hakuna wanafunzi shuleni, shule, vyuo na maofisi hufungwa, watu hulazimika kuyakimbia makazi na hakuna anayeweza kuwa na uhakika kama anaweza kukutana na ndugu zake tena wakiwa hai.
Vurugu hasa za wenyewe kwa wenyewe iwe ni kwa sababu zenye tija au la, hazijawahi kuiacha jamii salama. Tunawakumbusha Watanzania kwamba, vurugu zinapotokea waathirika wakubwa ni wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Hivyo, watu hawa ni ndugu, jamaa na marafiki kutokana na ukweli kwamba asilimia kubwa ya Watanzania ni ndugu.
Tunaungana na viongozi wa dini ambao tangu mchakato wa Uchaguzi Mkuu uanze, wamekuwa wakihubiri amani na kuisisitiza jamii kuhakikisha shughuli zote za uchaguzi na baada ya uchaguzi, nchi inabaki na amani.
Katika dunia ya leo, hakuna nchi nyingine iliyofichika inayoitwa Tanzania ambayo raia wa Tanzania ya leo wanaweza kukimbilia huko kwa uhuru kuishi, ikiwa amani yao itapotea.
Kwa msingi huo, tunashauri Watanzania wasikubali kwa namna yoyote kutumika au kufuata mkumbo wa kushiriki matendo ya kuhatarisha amani, bali wajikite katika kuilinda kwa mustakabali mwema wa Tanzania ya leo na ya kesho, kizazi cha sasa na kijacho.
Amani ya Tanzania iliyojengwa katika misingi ya ucha Mungu inawezekana, tuitunze leo ili itutunze kesho.