INEC yaagiza mambo 11 upigaji kura

DAR ES SALAAM; TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa maelekezo 11 ya kuzingatiwa katika vituo vya kupigia kura leo.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele alisema vituo vya kupigia kura vitafunguliwa leo saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.

Jaji Mwambegele alisema jana kuwa vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 9:00 alasiri.

“Mpigakura yeyote atakayekuwepo kwenye mstari kituoni wakati wa kufungwa kwa kituo ataruhusiwa kupiga kura. Mlinzi wa kituo atasimama nyuma ya mpiga kura wa mwisho kuhakikisha wanaopiga kura ni wale waliowasili kabla ya muda wa kufungwa, wataendelea kupiga kura hadi wapigakura wote watakapomaliza,” alieleza.

Jaji Mwambegele alisisitiza kwamba hairuhusiwi kuvaa sare za vyama vya siasa, kuendesha kampeni au kukaa ndani ya meta 300 kutoka kituo cha kupigia kura siku ya uchaguzi.

Taarifa ilieleza kwamba mpigakura atakayeshindwa kutambua kituo chake, atasaidiwa na karani mwongozaji kwa kutafuta jina lake kwenye orodha na kumwelekeza kituo husika.

Aidha, alisema wapigakura walioko kwenye mstari wanaotakiwa kupewa kipaumbele ni watu wenye mahitaji maalumu kama wazee, wagonjwa, watu wenye ulemavu, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha.

“Kwa wapigakura wasioona lakini wanaoweza kusoma maandishi ya nukta nundu, watapewa fursa ya kutumia jalada la nukta nundu kupiga kura wenyewe. Wale wasioweza kutumia jalada hilo, wataruhusiwa kwenda na mtu wanayemwamini ili kuwasaidia kupiga kura,” alieleza Jaji Mwambegele.

Taarifa ilieleza kwamba, kila mtu anatakiwa kupiga kura yake kwa siri bila kushawishiwa na mtu yeyote kwa kueleza ni nani amempigia kura.

Baada ya kupiga kura, wapigakura wanatakiwa kuondoka vituoni na kurejea nyumbani, kwa kuwa mawakala wa vyama vya siasa watakuwepo kulinda maslahi ya wagombea wao.

“Baada ya upigaji kura kukamilika, hatua ya kuhesabu kura itafanyika katika kituo husika cha kupigia kura. Endapo kutatokea changamoto, kuhesabu kura kunaweza kufanyika katika eneo lingine na mawakala wa vyama vya siasa watashuhudia hatua zote za kujumlisha matokeo kuanzia vituo vya kata, majimbo hadi makao makuu ya tume ambapo matokeo yatatangazwa rasmi na mshindi kutangazwa,” alieleza Jaji Mwambegele.

Alisema mpigakura atapiga kura katika kituo alichojiandikisha au alichopangiwa na INEC na kwamba yeyote aliyebadilisha taarifa zake kwenda kituo ambacho hakujiandikisha na ambaye aliomba kupiga kura ya Rais pekee, hataruhusiwa kupiga kura katika kituo alichojiandikisha awali kwa kuwa jina lake halitaonekana katika kituo hicho.

Jaji Mwambegele alisema wagombea wa urais ni 17 ambao kati yao, wanawake ni watatu sawa na asilimia 17.65 na wanaume 14 sawa na asilimia 82.35. Kwa nafasi ya makamu wa Rais, wanawake ni tisa sawa na asilimia 53 na wanaume wanane sawa na asilimia 47.

Alisema kuna wagombea wa ubunge 1,729 ambao kati yao, wanawake ni 558 sawa na asilimia 32 na wanaume 1,171 sawa na asilimia 68.

Idadi ya watu wenye ulemavu ni 27 sawa na asilimia 1.56. Wagombea wa udiwani ni 7,239, kati yao wanawake ni 718 sawa na asilimia 10, wanaume 6,521 sawa na asilimia 90 na wenye ulemavu 57 sawa na asilimia 0.79.

Jaji Mwambegele alisema vituo 99,895 vitatumika kupigia kura, kati ya hivyo 97,348 viko Tanzania Bara na 2,547 Zanzibar.

“Jumla ya majimbo 272 yatahusika, kati yake 222 ni Bara na 50 Zanzibar na kata kwa ajili ya madiwani Tanzania Bara ni 3,950. Katika uchaguzi wa wabunge ni majimbo 270 yatakayofanya uchaguzi,” alisema

Jaji Mwambegele alivipongeza vyama vya siasa na wagombea waliojitokeza na walioteuliwa kugombea nafasi ya kiti cha rais na makamu wa rais, ubunge na udiwani.

“Kwa namna ya kipekee, nivipongeze vyama vyenye wagombea, wagombea wao, wanachama, wapenzi, wafuasi na mashabiki wao kwa kufanya kampeni za kistaarabu na kuzingatia Kanuni za Maadili ya Uchaguzi za Mwaka 2025,” alisema.

Aliongeza: “Nawapongeza wananchi wote kwa utulivu mliouonesha wakati wote wa kipindi cha kampeni. Kwa kiasi kikubwa, kampeni zimefanyika kwa utulivu na amani na pale palipojitokeza kasoro ndogondogo katika kampeni hizo, kamati za maadili katika kila ngazi zilishughulikia malalamiko hayo kwa ufanisi mkubwa”.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. JOIN US Everybody can earn 250/h Dollar + daily 1K… You can earn from 6000-12700 Dollar a month or even more if you work as a part time job…It’s easy, just follow instructions on this page, read it carefully from start to finish… It’s a flexible job but a good earning opportunity. tab for more detail thank you……..

    .

    This is my main concern……………………………………. http://Www.Cash43.Com

  2. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us →→→→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button