Tanzania yaihakikishia dunia usalama wa watalii

DODOMA: Wizara ya Maliasili na Utalii imeutaarifu umma kuwa wageni na wadau wa Sekta ya Utalii ndani na nje ya nchi, kwamba hali ya amani na utulivu imerejea na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zinaendelea baada ya kudhibitiwa kwa vurugu zilizoibuka Oktoba 29, hadi Novemba 1, 2025.
Wizara hiyo imeeleza Tanzania kama Mwanachama wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), inatekeleza na kusimamia Mwongozo wa Utalii Kimataifa unaoelekeza nchi kuhakikisha usalama wa wageni, ikiwemo wasafiri na watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali wawapo nchini.
Vituo vyote vya kuingia na kutoka nchini kupitia usafiri wa anga, barabara, maji, reli, sambamba na usafiri wa umma vinaendelea kutoa huduma kwa utaratibu wa kawaida. Aidha, shughuli za utalii na huduma kwa wageni zinaendelea kutolewa katika maeneo yote nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Wasafiri wanahimizwa kuendelea na mipango yao ya kutembelea na kufurahia vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Tanzania bila hofu yoyote. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuwa nchi salama, yenye utulivu, na mazingira rafiki kwa shughuli zote za usafiri, uwekezaji kibiashara na utalii; hivyo,Serikali inachukua fursa hii kuwakaribisha wageni wote nchini.



