TEF yawasihi Watanzania kuimarisha umoja, amani

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limewaomba wananchi kusimama pamoja kama taifa, kuzungumza na kujisahihisha, ili vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu zisitokee tena. Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ilieleza jukwaa linafuatilia kwa karibu na limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Watanzania, wakiwamo wanahabari na wengine waliojeruhiwa.
Ilieleza jukwaa linarejea utamaduni wa taifa wa kuwa na amani, utulivu na kuakisi yaliyotokea yakazaa maafa hayo. “Tunafahamu yapo maumivu makubwa kila upande, ila tunaomba sasa tusimame pamoja kama taifa, tuzungumze na kujisahihisha, ili kamwe haya yasitokee tena katika ardhi ya Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa TEF inatoa mwito kwa mamlaka kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha haki inatendeka na kuitaka serikali kuanzisha mchakato wa maridhiano haraka ili kuponya majeraha kwa pande zote, kuomba kila upande mchakato huo utakapoanza uwe tayari kushiriki kama nchi kumaliza kadhia hiyo.
Aidha, TEF imetoa pole kwa Watanzania waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu kwa kile kilichoanza kama maandamano ya amani, lakini kuishia kwenye uchomaji wa magari, vituo vya mafuta, nyumba, kadhia zingine za kiafya kwa waliopiga kura na mauaji ya raia na askari.
Taarifa hiyo imeeleza siku ya tukio walipokea taarifa za vifo vya vijana na askari polisi kwa sababu baadhi ya wananchi waliwasiliana na wahariri, kuomba msaada wa kuulizia walipo ndugu zao. “Jukwaa linawakumbuka kwa heshima wanahabari na Watanzania waliouawa katika vurugu hizo, kwani wameacha pengo kubwa katika tasnia ya habari, kazini na familia zao. Pia linawapa pole wote waliojeruhiwa katika matukio hayo,” imeeleza. SOMA: THBUB yalaani vurugu za uchaguzi mkuu



