Kuapishwa Leo Ikulu Chamwino

RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kumuapisha Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka imeeleza Dk Mwigulu ataapishwa saa nne asubuhi katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. Rais Samia aliteua jina la Waziri Mkuu kutekeleza Ibara ya 51 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Toleo la 2005.

Ibara ya 51(1) ya katiba hiyo inamtaka Rais ateue mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi bungeni. Katiba inaeleza kama hakuna chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi, atateuliwa Waziri Mkuu anayeelekea kuungwa mkono na wabunge walio wengi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari alilieleza Bunge kuwa Dk Mwigulu ana sifa za kuwa Waziri Mkuu kwa kuwa ni mchapakazi, msikivu na ana upeo wa mambo. Johari alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati akitoa hoja ya serikali kabla ya wabunge kupiga kura.

Amesema Dk Mwigulu ni mchumi mbobevu mwenye shahada ya uzamivu katika masuala ya uchumi. “Kwa uzoefu na ubobevu huu wa taaluma, ni mtu sahihi kwa nafasi hii ya Waziri Mkuu.

Ni mtu mwenye busara nyingi, ni msikivu wa hali ya juu. Anapokumbana na tatizo lolote, anashaurika na hupokea ushauri kwa mikono miwili,” alisema Johari. Alisema Dk Mwigulu ana uwezo wa kuchambua na kupima hoja na ana uelewa wa mambo katika kufikia maamuzi umejidhihirisha katika utumishi wa umma. “Naziwasilisha sifa hizi ili sote kwa pamoja tumthibitishe kuwa ni mwenye uwezo wa kuyabeba majukumu yanayoendana na wadhifa wa Waziri Mkuu, kwani anaweza kuyahimili,” alisema Johari.

Dk Mwigulu aliingia kwenye siasa kwa kuwa mbunge mwaka 2010 hadi sasa. Katika kuonesha kuaminiwa kwake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ndani ya serikali, ameshika nyadhifa mbalimbali. Dk Mwigulu aliwahi kuwa Mhazini wa CCM tangu mwaka 2011 hadi mwaka 2012 na pia alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM mwaka 2012 hadi 2015. SOMA: Rais Mwinyi atangaza Baraza Jipya la Mawaziri

Kwa upande wa serikali, aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kipindi kifupi mwaka 2016 na baadaye akahamishiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi hadi mwaka 2018. Mwaka 2020 aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, wadhifa ambao alikuwa nao mpaka wakati anateuliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button