Upinzani wampongeza Dk. Mwigulu

WABUNGE wa vyama vya upinzani wameeleza matarajio yao kwa Waziri Mkuu mteule, Dk Mwigulu Nchemba ukiwemo usimamizi wa rasilimali za taifa ili ziwaletee wananchi maendeleo. Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu kupitia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) amesema hayo bungeni Dodoma kwa niaba ya wabunge wengine wa vyama vya upinzani, baada ya Dk Mwigulu kutangazwa kupendekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan awe Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shaibu amesema kwa niaba ya wenzake wachache waliopo bungeni, waliunga mkono hoja hiyo ya pendekezo la uteuzi wa Dk Mwigulu kuwa Waziri Mkuu. Amesema mbali na sifa zote zilizoainishwa na wazungumzaji wengine bungeni hapo, upande wao hawakuwa na shaka kuwa sifa moja ambayo inaweza kuwa imemsukuma Rais Samia kumteua Dk Mwigulu ni uchapakazi.
“Sisi tulio wachache tunapenda kusema bayana kwamba tunakuunga mkono kama ishara ya kukukopesha imani, tukiwa na uhakika kwamba utachapa kazi na maeneo ya matarajio yetu ni mengi sana,” alisema Shaibu. SOMA: Tunamtakia utendaji uliotukuka Dk. Mwigulu
Amesema imani yao ni kwamba,Dk Mwigulu atakwenda kuwajibika na mambo mbalimbali kwa manufaa ya wengi na wana imani atasimamia serikali katika usimamizi wa rasilimali za taifa katika kuwaletea wananchi maendeleo. Pia, wamesema wanatarajia kuwa atasimamia maboresho ya demokrasia nchini na kulipatia taifa katiba mpya, kwa kuzingatia tasnia ya siasa na vyama vya siasa kwa ujumla wake vipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Ameongeza kuwa, imani yao ni kwamba ataongoza mapambano ya kushughulikia changamoto za kiuchumi na za kijamii zinazowakabili Watanzania, yaani hatokuwa Waziri Mkuu wa ofisini, bali wa vitendo kama ilivyo desturi.




HONGERA MHE. DKT
MWIGULU
https://www.youtube.com/watch?v=dF54MTFUgkc
https://www.youtube.com/watch?v=8No-vwV5ZoA
https://www.youtube.com/watch?v=b4Tysva80Ms
https://www.youtube.com/watch?v=0SggxPDsYWI
https://www.youtube.com/watch?v=rVUTwaOq_28
https://www.youtube.com/watch?v=2TXoRfRabtM
https://www.youtube.com/watch?v=8RcImu8osyw