Serikali ya kasi

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaapisha mawaziri na naibu mawaziri huku akiwataka kutenda kazi kwa kwenda mbio na kutafuta fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri 27 na Naibu mawaziri 29 katika Ikulu ya Chamwino, Rais Samia amesema changamoto iliyopo ni uchache wa rasilimali fedha za ndani na kuwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kutafuta fedha za ndani ili kutekeleza miradi hiyo.

“Changamoto inayotukabili ni rasilimali, rasilimali zetu ni chache, kama mnavyojua mara nyingi tunategemea kupata kutoka nje, mikopo kutoka kwa taasisi mbalimbali za kimatifa na benki za kimataifa,” amesema.

Ameongeza: “Lakini yaliyotokea (vurugu wakati wa uchaguzi) nchini kwetu yametutia doa kidogo na huenda yakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza wa awamu ya sita, muhula wa kwanza tulikuwa tunapata sana, kwa sifa zetu, kwa msimamo wetu na kwa kazi tunazofanya, lakini doa tulilojitia linaweza likaturudisha nyuma.”

“Kwa maana hiyo tuna kazi ya kutafuta fedha humu ndani, kutumia rasilimali zetu alizotupa Mungu, tutaangalia njia gani tutazitumia tupate fedha ili tutekeleze miradi ambayo tunakwenda kuitekeleza,” ameeleza.

Rais Samia amesisitiza kuwa muhula wa pili wa uongozi wake, serikali imejipanga kuanza kutekeleza miradi kwa fedha za ndani bila kusubiri za wahisani.

“Mambo ambayo tumeahidi kwa wananchi wetu ni mengi na muda wa kuyatekeleza ni mchache sana, kwa hiyo wale mlioapa leo (jana) aliye mzito akapunguze kilo kidogo, tunatakiwa kwenda mbio na ni mbio hasa,” alisema.

“Kubwa zaidi muhula wa pili wa awamu ya sita tutaanza kufanya miradi wenyewe halafu mashirika yatatukuta njiani, hatutakaa tusubiri, tunauza mradi na kwenda kubembeleza kukiwa na masharti mengi, badala ya kupata mkopo kwa miezi mitatu au minne unachukua mwaka mzima tunabembeleza mradi mmoja mpaka kibali kinatoka tuna miaka miwili tumemaliza. Hatutasubiri hayo, tutaanza kwa fedha ya ndani halafu… watatukuta
katikati, huo ndio mwelekeo,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Na huo sio wajibu wa rais pekee yake, ni wajibu wetu sote, Makamu wa Rais (Dk Emmanuel Mchimbi) anasikia, Waziri Mkuu (Dk Mwigulu Mchemba) anasikia, Spika wa Bunge (Mussa Azzan Zungu) na wabunge wanatusikia, kwa hiyo ndio mwendo tunakwenda nao”.

Aidha, Rais Samia alionya mawaziri na naibu mawaziri walioapa jana kuwa hatosita kuwaondoa kwenye nyadhifa zao pindi atakapobaini wameshindwa kuwajibika katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Amesema viongozi hao hawapaswi kujionea fahari kushika nyadhifa hizo kwani wapo wabunge wengine wenye sifa za kutosha, hivyo aliwataka kutimiza majukumu ya kulihudumia taifa ipasavyo.

“Tuko hapa kuwashuhudia mkikubali kubeba majukumu, tuko hapa kugawana majukumu, mmeapa na wizara zenu na hayo ndio majukumu ambayo mmekubali kubeba na ni imani yangu kwamba mmeyabeba kwa moyo mkubwa, mmeyabeba kwa moyo kwamba tunakwenda kuwatumikia watu,” alisema.

Ameendelea, “Majukumu tuliyopeana leo (jana), dhamana tulizopeana ni dhamana za kazi na si fahari kwamba na mimi ni waziri ikiwa ndio ufahari, ulikotoka, unakokaa na kwingineko hapana, tumebeba majukumu ya kwenda kuwatumikia wananchi.”

“Kama ilivyo kauli mbiu ya Kazi na Utu, tunasonga mbele, ule utu uanze na sisi wenyewe viongozi mawaziri, naibu mawaziri ambao tunakwenda kuwasimamia wengine, ukiangalia neno utu lina maana pana sasa, kwa maana yoyote ile utu uanze na sisi halafu tuoneshe utu kwa watu wetu, kujenga utu wao, kuheshimisha utu wao, utu wa mtanzania hiyo ndio kazi yenu.

“Sasa kwa wale ambao watabeba uwaziri kama fahari, nimeapa na mimi leo (jana), nimeukwaa watanijua mtaani basi tutafuatana polepole, na sisi tutakuwa nyuma yenu,” alisema.

Rais Samia alisisitiza, “Miaka mitano si midogo lakini si mingi sana, mimi sioni shida kubadilisha na mnanijua… nitabadilisha mpaka nimpate yule aliye tayari kufanya kazi na mimi kwa moyo mkuu na kwa moyo mmoja.”

Amehimiza pia umuhimu ni kuwajibika kwa Watanzania kwani yapo mengi yaliyoahidiwa lakini muda wa utekelezaji wake ni mchache. “Kwa hiyo ndugu zangu mawaziri kazi yetu hapa kuanzia leo ni kuwajibika kwa wananchi, ni kuwajibika kwa taifa ni kuwajibika kwa nchi yetu Tanzania,” alisema.

Rais Samia pia aliwataka kuhakikisha wanaanza sasa kutekeleza yale yaliyoahidiwa kwa wananchi ikiwamo yale aliyoahidi kuyatekeleza ndani ya siku 100.

“Kwa mlioapa leo ambao ahadi ya siku 100 zinagusa wizara zenu, makatibu wakuu hawajabadilika, mkaungane nao kuzichambua na kuanza kuzitekeleza,” alisema.

Rais Samia pia alisema hataki kusikia kauli za michakato ya utekelezaji wa miradi kutokamilika na kusisitiza kuwa anachotaka kuona ni matokeo chanya ya miradi.

“Sitaki kusikia tunaendelea, tuko mbioni nataka matokeo kwa wananchi. Tukikubaliana mradi nataka matokeo na sio matokeo ofisini kwako, sitaki tumefikia hapa, bado hapa Hapana, nataka matokeo kwa wananchi kwa yale tuliyokubaliana,” alisema.

Aliongeza: “Kwanza niwape pole kwa kazi nzito iliyo mbele yetu, lakini pia niwapongeze kwa kuapa, kuna wabunge zaidi ya 390 lakini ninyi ndio mmeibuka kumsaidia rais kwenye wizara tulizogawana. Si kwamba ni wazuri kuliko wengine wote kule ndani, vigezo vilikuwa vingi hivyo mkafanye kazi”.

Katika hotuba yake, Rais Samia aliwashukuru waliokuwa mawaziri katika muhula wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya kazi zilizoleta maendeleo.

“Lakini kazi ni kupishana, tuna timu mpya kongwe wamechanganyika tukaendeleze mapambano ya kuwaletea maendeleo wananchi,” amesema.

Rais Samia alisema leo kutakuwa na kikao kazi cha viongozi hao ambapo masuala mbalimbali wataelezwa kuhusu hali ya uchumi, rasilimali na mikakati ya kitaifa.

Hali ilivyokuwa
Viongozi na wageni mbalimbali walianza kuwasili Ikulu kuanzia saa 3:00 asubuhi ambapo ilipofika saa 5:13 asubuhi, mawaziri walianza kula kiapo.

Mawaziri na naibu mawaziri waliokuwa wamevalia suti za rangi nyeusi na buluu iliyoiva, wa kwanza kula kiapo hicho ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Wenye ulemavu, William Lukuvi.

Shughuli ya uapisho ilichukua dakika 104 na kuhitimishwa saa 6:53 mchana kwa Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba kula kiapo ambapo baada ya tukio hilo Kamishna wa Maadili, Jaji Sivangilwa Wangesi aliongoza kiapo cha maadili kwa mawaziri hao.

Baada ya kiapo hicho, Jaji Wangesi aliwataka mawaziri hao kuweka saini katika hati za viapo walivyokula, tayari kwenda kuwatumikia wananchi.

Maoni ya mawaziri
Waziri wa Viwanda, Judith Kapinga alisema agizo la Rais Samia kuhusu kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani limewapa angalizo na kuwatoa hofu Watanzania kuwa hakuna kitakachokwama.

“Kwa wizara yangu kunatakiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambavyo vitakwenda kutoa ajira na kuinua uchumi, lakini ikishindikana kupata fedha kinachosimama ni maarifa.

“Wizara ya Viwanda ni injini ya uchumi, zile ajira milioni nane kwenye Ilani ya CCM nyingi zinapaswa kuzalishwa na viwanda, kwa sababu hiyo ni lazima tuendelee kukimbia kwa kutumia akili na maarifa yetu ili tufanikiwe,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Regina Ndege alisema tafsiri ya Kazi na Utu ndiyo kipimo kikubwa cha utumishi kipindi hiki.

Regina alisema malengo ya rais yatatimia ikiwa mawaziri, naibu mawaziri na makatibu wakuu watafanya kazi na ushirikiano kuliko kutanguliza maslahi binafsi na juu yake wasitanguliza maslahi binafsi.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alisema, “Miradi mingi inayotekelezwa katika wizara yangu inataka fedha na Rais Samia anataka matokeo.

Hivyo katika kuzifungua barabara tutategemea kutumia akili zaidi na maarifa ili tuepuke sababu za ukamilishwaji wa miradi, lakini niwahakikishie hakuna linaloshindikana ndani ya wizara na Watanzania wategemee matokeo”.

Akizungumzia kauli hiyo na maagizo ya kuwataka mawaziri wakimbie, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema imani aliyopewa na rais ni kubwa hivyo yaliyoagizwa lazima akayatimize kwa nguvu na maarifa zaidi.

“Milango ya kutekeleza miradi itafunguka na wanyonge wataendelea kupata haki yao kama ilivyokuwa ikitarajiwa,” alisema.

Habari Zifananazo

13 Comments

    1. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
      .
      M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us →→→→→→→ https://Www.Work27.Online

    2. I get paid over (90$ to 500$ / hour ) working from home with 2 kids at home. I never thought I would be able to do it but my best friend earns over $22000 a month doing this and she convinced me to try. it was all true and has totally changed my life… This is what I do, check it out by Visiting Following web….
      .
      HERE——————————————⊃⫸ http://Www.Cash43.Com

    3. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
      .
      M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→→→→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button