Viongozi watakiwa kupambana wizi wa umeme

VIONGOZI wa serikali za mitaa na madiwani wametakiwa kuwa mstari wa mbele kupambana na wizi wa umeme ili kuzuia uharibifu mkubwa wa miundombinu na hasara kwa taifa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alisema hayo jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mafunzo kwa viongozi wa ngazi za mitaa na kusema wajibu wa kiongozi ni kuhakikisha anafuatilia matukio ya uunganishaji holela wa umeme na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika.

“Tuna jukumu la kuhakikisha tunakuwa macho katika maeneo yetu na kuibua matukio ya wizi wa umeme. Watu wanajenga, wanavunja majengo, lakini bado wanajiunganishia umeme kiholela. Hii ni hatari kubwa kwa usalama wa miundombinu yetu,” alisema Mpogolo. SOMA: Polisi yadaka wezi wa magari, bajaji

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa mitaa, madiwani na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata huduma za umeme kwa usalama na ufanisi, hasa katika maeneo mapya ya ujenzi kama Kariakoo na maeneo mengine ya Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle alisema mafunzo hayo yameshirikisha viongozi wa serikali za mitaa kutoka wilaya za Ilala, Temeke na Kigamboni, lengo likiwa ni kuimarisha mahusiano na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa mkoani Dar es Salaam, Juma Abbasi aliipongeza Tanesco kwa hatua wanazochukua kuboresha huduma za umeme nchini, akisema ushirikiano kati ya shirika hilo na serikali umechangia kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button