Usugu wa dawa tishio kwa watoto

USUGU wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa umetajwa kuwa tishio kubwa kwa watoto wenye umri mdogo kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya viuavijasumu. Takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa Tanzania inakabiliwa na zaidi ya vifo 10,000 vinavyotokana moja kwa moja na usugu huo, huku zaidi ya vifo 55,000 vikihusishwa na tatizo hilo kimazingira na kimatibabu.
Aidha, kati ya vifo hivyo, takribani 17,000 hutokea kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa ifikapo mwaka 2050, dawa nyingi zinaweza kushindwa kutibu wagonjwa kutokana na kuongezeka kwa vimelea sugu, hali inayotokana na matumizi yasiyo sahihi ya antibayotiki kwa binadamu na mifugo.
Akizungumza na Daily News Digital, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Mary Kisima, amesema Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Usugu wa Dawa barani Afrika litakalofanyika Desemba 2–6, 2025. SOMA: Matumizi holela ya dawa sababu usugu wa tiba

Amesema maadhimisho ya Wiki ya Usugu wa Dawa yalianza Novemba 18–24, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu chanzo na madhara ya tatizo hilo. Kisima amesema usugu wa dawa unaweza kusambaa kutoka mtu hadi mtu kupitia mazingira yasiyo safi, ikiwamo matumizi ya vyoo na kushindwa kusafisha maeneo husika.
Kwa upande wake, Mfamasia wa Binadamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Samson Misinzo, amesema duniani kuna takribani vifo milioni 1.1 vinavyosababishwa moja kwa moja na vimelea sugu, na zaidi ya vifo milioni 4.7 vinahusishwa na usugu huo kila mwaka.
Amesema Afrika inachangia sehemu kubwa ya vifo hivyo, hususan nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zikiwamo Tanzania, na kusisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kudhibiti matumizi mabaya ya dawa ili kupunguza madhara ya kiafya na kiuchumi kwa wananchi.



