Tinubu atangaza dharura ya usalama

RAIS wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ametangaza hali ya dharura ya usalama wa kitaifa kufuatia kuongezeka kwa matukio ya mauaji, utekaji nyara na mashambulizi katika majimbo kadhaa nchini humo.

Kupitia amri hiyo maalumu, serikali imeviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza maafisa wapya 20,000, hatua itakayofanya jumla ya maafisa watakaohusika katika operesheni za kukabiliana na uhalifu kufikia 50,000.

Rais Tinubu amesema kuwa kambi za Huduma ya Taifa kwa Vijana (NYSC) zitatumika kama vituo vya muda vya kutoa mafunzo, ili kuharakisha maandalizi ya maafisa watakaotumwa katika maeneo yenye changamoto za usalama. SOMA: Rais Tinubu atangaza hali ya hatari Rivers

Kwa upande wa misitu, serikali imeipa mamlaka Idara ya Usalama wa Taifa (DSS) kupeleka mara moja walinzi wa misitu walio tayari kukabiliana na magaidi na makundi ya kihalifu yanayojificha misituni, sambamba na kuajiri walinzi wengine zaidi ili kuimarisha ulinzi na operesheni za kuwasaka wahalifu.

Hatua hiyo imekuja kufuatia matukio ya hivi karibuni ya utekaji nyara wa wanafunzi na raia, yakiwamo ya wanafunzi wa Shule ya Kanisa Katoliki ya Mtakatifu Mary, iliyopo Jimbo la Niger. Serikali imesisitiza kuwa itaendelea na jitihada za kuwaokoa na kuwalinda waathirika wote.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button