Zaidi ya 40 wapoteza maisha Hong Kong

ZAIDI ya watu 40 wamethibitishwa kufariki dunia katika moto mkubwa ulioteketeza majengo kadhaa ya ghorofa jijini Hong Kong. Watu wengine 45 wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya, huku zaidi ya 279 wakiripotiwa kutopatikana hadi sasa.
Polisi wamewakamata watu watatu kwa tuhuma za mauaji, wakiwemo wakurugenzi wawili wa kampuni ya ujenzi na mshauri mmoja wa masuala ya uhandisi. Wakati uchunguzi wa chanzo cha moto huo ukiendelea, polisi wamegundua wavu na makaratasi ya plastiki yalipatikana yakifunika madirisha ya majengo wakati wa ukarabati huenda ikawa chanzo cha moto huo kuenea kwa kasi .
Mapema leo Novemba 27, moshi ulikuwa bado unafuka kutoka baadhi ya majengo, ingawa moto umedhibitiwa katika majengo manne kati ya manane.Idara ya Zimamoto ya Hong Kong imesema inaweza kuchukua siku nzima kuuzima moto huo kikamilifu.
Mamia ya wakazi wamehamishwa na kupelekwa kwenye makazi ya muda pamoja na nyumba za dharura zilizotengwa kwa walioathrika na moto huo. Kwa mujibu wa Idara ya Zimamoto, huu ni moto mkubwa zaidi kuwahi kutokea Hong Kong katika kipindi cha miaka 17. SOMA: Jamii yaagizwa kuchukua tahadhari ya moto



