Mavunde abainisha mikakati kuimarisha biashara ya Tanzanite nchini

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Serikali imejipanga upya kuitangaza na kuiinua Tanzanite kimataifa kupitia mkakati wa kurejesha hadhi ya jiwe hilo adimu duniani.
Akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini ya vito katika eneo tengefu la ukuta wa Magufuli, Mirerani mkoani Manyara, Waziri Mavunde amesema hatua hiyo inalenga kurejesha hadhi na uhitaji (*rebranding* )wa Tanzanite ili kuimarisha thamani na soko lake duniani.

Katika Mkutano huo ambao pia ulihusisha hafla ya kukabidhi leseni kwa wanufaika 423, Waziri Mavunde amesema Serikali imedhamiria kurejesha minada ya madini ya vito kama njia ya kuongeza uwazi, ushindani na thamani ya madini ya vito nchini.
Akifafanua zaidi, amesema Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa Tanzanite Exchange Centre (TEC), jengo ambalo hadi sasa limefikia asilimia 98 ya ujenzi katika ghorofa mbili na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kituo hicho kianze kufanya kazi mapema na kutumika kama kitovu cha kimataifa cha biashara ya Tanzanite.

“Tunataka wageni wanaokuja kununua Tanzanite wapate huduma zote muhimu katika eneo moja, kuanzia huduma za kibenki, hoteli, hadi miundombinu rafiki ya biashara,” amesema Mavunde.
Pia, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuona Mirerani, Arusha na maeneo mengine nchini yanakuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito barani Afrika.

“Rais Samia anataka kuona ‘ mfumo wa biashara ya madini ya vito kama ilivyo Hong Kong na Dubai ikihama na kuja hapa Simanjiro,”amesema.
Akitaja changamoto kubwa kwa wachimbaji wadogo, Waziri Mavunde amesema Serikali inafanya mazungumzo na Wizara ya Fedha kuwezesha upatikanaji wa mitaji kupitia mifuko ya dhamana.



