Barrick yakabidhi leseni 13 kwa wachimbaji wadogo Tarime

MGODI wa Barrick North Mara umetoa leseni 13 na kufadhili mafunzo kwa wachimbaji wadogo ili waendeshe shughuli za uchimbaji. Mgodi huo uliopo Nyamongo wilayani Tarime umetoa leseni hizo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi wa serikali wa kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kufanya uchimbaji wa kisasa na wenye tija.
Mradi huo unaolenga kunufaisha vijana zaidi ya 2000, wanawake na wenyeulemavu uliozinduliwa Mei mwaka huu upo chini ya programu ya serikali ambayo itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu hadi 2030.
Awali, serikali ilikabidhi leseni 48 za uchimbaji kwa vikundi vya walengwa. Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Amini Msuya alisema kupitia ushirikiano na Barrick North Mara, tayari mamia ya vijana walengwa wamepatiwa mafunzo ya awali ya kushiriki katika mradi kwa kufanya uchimbaji wa kisasa na wenyetija.

“Tunaendelea kuwahakikishia wachimbaji wadogo wa madini kutoka vijiji vilivyo jirani na mgodi wa dhahabu wa North Mara kuwa mradi huu utakuwa wa mfano kwa Tanzania na pengine hata kwa Afrika kwa ujumla, kwa kuwa umelenga kuhakikisha makundi mbalimbali katika jamii yanamiliki migodi na kunufaika na biashara ya madini,” alisema.
Msuya amesema kwa sasa mradi umefikia hatua ya utafiti zaidi na maandalizi ya mpango na bajeti ili kazi ianze kwa mafanikio. Ametoa wito kwa walengwa kuendelea kuwa wavumilivu na kuwasiliana na ofisi yake wanapohitaji ufafanuzi wa jambo lolote au kutoa ushauri kuhusiana na mradi huo. “Wachimbaji wadogo waendelee kuamini serikali pamoja na mgodi wa Barrick North Mara kwa kuwa ipo dhamira ya kweli yakuhakikisha wananufaisha na mradi huu” alisisitiza,” alisema Msuya.

Wakati wa uzinduzi wa mradi huo Mei, mwaka huu serikali kupitia Wizara ya Madini ilieleza kuwa hatua hiyo ni uekelezaji wa programu ya kuongeza faida za uchimbaji madini (MBT) na kuwa mradi huo wa kihistoria na wa kwanza kufanyika nchini baina ya serikali, mgodi na wananchi wanaozunguka mgodi. Novemba 14, wakati akizindua Bunge la 13 jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo serikali itandelea kutekeleza mipango ya kuwanufaisha Watanzania na taifa kwa ujumla kupitia sekta ya madini.
Naye Meneja wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema kampuni imetoa leseni hizo kwa lengo la kuimarisha uhusiano mwema na jamii



