…Aagiza Polisi wasimtafute Askofu Gwajima

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi liache kumtafuta Askofu Dk Josephat Gwajima. Dk Mwigulu amesema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Arumeru katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Magufuli Leganga, Kata ya Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Amesema baada ya kutoa msamaha kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima, waumini wanahitaji wamuone kiongozi wao hivyo anatakiwa ajitokeze hadharani aendelee na kazi yake. “Mwacheni ajitokeze tujenge umoja wa kitaifa, tushikamane kurudisha umoja wa kitaifa. SOMA: Mwigulu: Tukatae kugawanywa

Tumekutana na TEC, viongozi wa dini, wa mila na viongozi mbalimbali; twendeni sote kwenye jambo hili, tujitokeze tuhamasishe Tanzania yenye amani, huu ndio wito wa kiongozi wetu wa nchi,” alisema Mwigulu. Ameongeza: “Twendeni sote Watanzania tuongee sote kwa pamoja kurudisha umoja wa Kitanzania, tukienda kwa njia hii iliyojitokeza hakuna atakayeshinda, tuseme lugha moja na kumtanguliza Mungu mbele”.

Kabla ya mkutano huo amekagua uharibifu uliofanywa wakati wa vurugu za Oktoba 29 mwaka huu kwenye Kituo cha Polisi cha Kikatiti (meta 500 kutoka barabara kuu ya Arusha – Moshi); Mahakama ya Mwanzo ya Maji ya Chai (kilometa 3 kutoka barabara hiyo kuu), kituo cha mafuta Total Energies kilichopo Maji ya duka kubwa na sehemu ya kutunzia fedha ilibomolewa.

Dk Mwigulu amesema masuala ya maendeleo ya wilaya ya hiyo kama vile maji na barabara yamo kwenye Ilani ya CCM na kwenye ahadi za Rais Samia lakini yatafanyika endapo tu nchi itakuwa na amani. “Tukichagua vurugu tutakuwa tumechagua kufukuza maendeleo, tukichagua vurugu tutakuwa tumechagua kuongeza umaskini kwa mtu mmoja mmoja,” alisema.

Ameongeza : “Kila Mtanzania akatae haya yaliyotokea juzijuzi. Tumechochewa, tumechonganishwa lakini wao wako nje, wanalipwa ili kutuvuruga tu. Wengi wanaochochea vurugu ni wanaharakati, wako nje ya nchi. Hakuna kiongozi wa chama cha siasa anasema wananchi wafanye vurugu. Au mmemuona?”

Amesema baadhi ya vijana walioko nje ya nchi wamebainika kupokea Dola za Marekani milioni mbili (sawa na Sh bilioni 4.5) ili wachochee vurugu. “Hawa watu wanalenga tugombane ili wachukue madini adimu. Sasa hivi Tanzania imegundua uraniumu ambapo inakuwa nchi ya tisa duniani na ya kwanza barani Afrika. Ina tani za ujazo 890,000.

Hii ni karibu tani milioni moja,” alisema Dk Mwigulu. Amesema  ziko baadhi ya nchi barani Afrika ziliathirika kutoka na chokochoko hizo. “Watanzania tuamkeni, tuchukue tahadhari. Kuna kamchezo kanachezwa. Wanajua Tanzania ina gesi asilia nyingi na inakaribia kuanza. Wanajua ikianza miradi hii, Tanzania itakuwa ya kwanza katika Afrika Mashariki na wala hatutahitaji kutoa mikopo ya wanafunzi,” alisema Dk Mwigulu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button