Sima achomoza umeya Mwanza
MWANZA; DIWANI wa Kata ya Mhandu, Sima Constantine ndiye Meya mpya wa Jiji la Mwanza.
Hatua hiyo inatokana leo kushinda kwenye kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), baada ya kupata kura 15 dhidi ya mpinzani wake Diwani wa Kata ya Nyegezi Happiness Ibassa aliyepata kura 11. Uchaguzi huo ulifanyika ofisi za CCM Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Nyamagana, Anita Rwezaura, alishinda nafasi ya Naibu Meya kwa kupata kura 14, huku wapinzani wake Mariam Shamte na Joyce Nyakiha kila mmoja akipata kura sita.

Meya huyo na Naibu wake sasa majina yao yatawasilishwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kesho kwa ajili ya kuthibitishwa, kwa vile hakuna diwani wa chama kingine zaidi ya CCM.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Sima amesema atashirikiana karibu zaidi na wananchi na madiwani wenzake kuleta maendeleo.
Kwa upande wake Naibu Meya mpya, Anita Rwezaura, amesema amejiandaa kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata matokeo chanya ya maendeleo.



