Kituo cha mabasi Ngangamfumuni kuifungua Moshi

MOSHI: UJENZI wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kimataifa cha Ngangamfumuni katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro unatajwa kuwa chachu ya kuibadilisha Manispaa hiyo na kuwa kitovu kipya cha shughuli za kiuchumi Kanda ya Kaskazini.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Maoinduzi (CCM)Taifa, Kenani Kihongosi amebainisha hayo leo Mei 30,2026 alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake mkoani humo ambao unagharimu jumla ya kiasi cha Sh bilioni 28.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo Kihongosi amesema kituo hicho hakitakuwa tu eneo la usafiri wa mabasi, bali pia kitakuwa kitovu cha biashara kitakachochochea ukuaji wa uchumi wa Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

Miongoni mwa fursa zitakazotokana na kituo hicho ni fursa za biashara, ajira na uwekezaji zinazotarajiwa kuzalishwa mara baada ya mradi huo kukamilika.
“Uwepo wa maduka, migahawa, huduma za kifedha, maeneo ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo, mama lishe na machinga ndani ya stendi hii utaongeza mzunguko wa fedha na kutoa fursa mpya za kipato kwa mamia ya wananchi wa Moshi,” amesema Kihongosi.
Kihongosi ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza mapato ya Manispaa ya Moshi kupitia ushuru, kodi na tozo mbalimbali zitokanazo na shughuli za usafiri na biashara zitakazoendeshwa katika kituo hicho.

Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwani tayari umeshapikea zaidi ya Sh bilioni 12 zilizowezesha kufufuliwa na kuendelea kwa ujenzi wake baada ya kusimama kwa muda kutokana na changamoto za kifedha.
Akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Mjini, Mwajuma Nasombe amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 28 na ulianza utekelezaji mwaka 2019 lakini ulisimama kutokana na changamito za kufedha zilizojirokeza.

Amesema pamoja na changamito hizo tayari Rais Samia ametoa kiasi cha Sh bilioni 12 kwa ajili ya kufucua mradi na kuendelea na utekelezaji na hadi sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake na mkandarasi ameongezewa muda hado Oktoba 26, mwaka huu ili kuukamilisha na uanze kutoa huduma kwa wananchi.



