Ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani kupata maendeleo

TANZANIA ni nchi iliyojaliwa uzuri wa kila namna.
Ina vivutio vingi vya utalii, madini, ardhi yenye rutuba inayokubali kila aina ya mazao na hali ya hewa nzuri inayomvutia mwanadamu yeyote kuishi.
Ni nchi iliyojengwa katika misingi ya raia wake kumuhofu Mungu, kufanyakazi kwa bidii, kutunza utu wa kila mtu na kulinda amani.
Ni kwa sababu hiyo, misingi hiyo tunashauri inapaswa kuendelea kulindwa kwa nguvu na juhudi kubwa ili rasilimali ilizojaliwa nchi hii ziweze kutumika kwa manufaa ya wote.
Tunasema hayo tukiamini kuwa, amani ndio msingi wa kila jema, hivyo ikiwa Watanzania tunataka maendeleo, ni lazima kuilinda amani ili shughuli na mipango hiyo iweze kutekelezeka.
Ipo miradi mingi imepangwa kutekelezwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2025-2030 na serikali iliyopo madarakani inayogusa maisha ya watu tena wa chini.
Miradi hiyo ni pamoja na wa kufikisha umeme kwa vitongoji vyote 64,359 ifikapo mwaka 2030 hata kabla ya hapo baada ya vijiji vyote 12,318 Tanzania Bara kufikishiwa umeme kwa asilimia 100.
Mradi huu unaotekelezwa na Wakala ya Nishati Vijijini (REA) ni mfano wa miradi mingi iliyotekelezwa na serikali kutokana na amani iliyopo nchini iliyowezesha kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP) linalozalisha megawati 2,115.
Tunafahamu ipo miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) inayoendelea kwa awamu nchini, ujenzi wa madaraja makubwa ya juu na ya chini, ujenzi wa barabara mijini na vijijini, vivuko, hospitali, shule na vyuo, haya yote yakitegemea amani.
Ndio maana tunaungana na viongozi wa serikali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, viongozi wa dini na jamii na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kwa yaliyotokea Oktoba 29, mwaka huu na kuzuia yasijirudie tena.
Tunawasihi Watanzania wote, mijini, vijijini na popote duniani walipo, kusahau tofauti za kiitikadi, kikabila na kidini kutambua kuwa Tanzania ni moja na tukikubali kuivuruga hatuna pakwenda na ukweli huu utusaidie kuilinda amani na nchi yetu kwa wivu mkubwa.
Tujenge umoja tulioachiwa na waasisi wa taifa hili, tuimarishe amani ili tuweze kutekeleza majukumu yetu ya kutuingizia kipato, watoto wasome na miradi ya maendeleo iendelee kutekelezwa.
Tunaamini tukiamua asiwepo wa kutuvuruga, tutailinda nchi hii na ushindi utakuwa wetu sote.



