Buchosa yapata Mwenyekiti halmashauri

MWANZA; HALMASHAURI ya Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza imepata uongozi mpya baada ya madiwani  kumchagua Isack Mashimba wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa kura 27 za ndiyo kati ya kura 28 zilizopigwa, ambapo kura moja ilimkataa.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, madiwani walimchagua William Samike wa CCM ambaye alipata kura zote 28 za ndiyo bila kupingwa.

Akizungumza leo mara baada ya kuchaguliwa, Mashimba aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na madiwani wote kuhakikisha wananchi wa Buchosa wananufaika na rasilimali nyingi zilizopo.

 

 

Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalumu, Magreth Kinyagwasa, alisema atashirikiana na uongozi mzima wa halmashauri kusimamia ipasavyo mapato ya ndani ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa haraka.

“Tutashirikiana na viongozi wote katika kuwatumikia wananchi. Buchosa ina vyanzo vingi vya mapato, tusimamie vizuri ili wananchi wanufaike,” alisema.

Kwa upande wake Diwani wa Nyazenda, Ibrahim Mbata, alisema atawekeza nguvu katika kuinua sekta ya elimu pamoja na kusimamia upatikanaji wa mapato kupitia rasilimali za halmashauri ikiwemo misitu na samaki.

Naye Diwani wa Ilenza, Micheal Edward, alisisitiza umuhimu wa usimamizi wa mapato ili kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande mwingine, Diwani wa Viti Maalumu, Zena Mbizo, aliahidi kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za halmashauri kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa uwazi na ufanisi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button