Mamkwe ahimiza ushiriki wa wanawake sekta za maendeleo

Kongwa, Dodoma: Wajiriwa wanawake wanaofanya kazi Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliungana na wenzao kuadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani katika maadhimisho yaliyofanyika wilayani Kongwa, mkoani Dodoma huku wakisisitiza ushiriki wa kundi hilo katika mnyororo wa thamani katika sekta za maendeleo.

Akizungumza mara baada ya maadhimisho hayo, Kaimu Mwenyekiti wa Wanawake wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Joyce Mamkwe amesema maadhimisho ya mwaka huu 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Haki na usawa kwa wanawake na wasichana, msingi jumuishi wa kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050’.

Amesema kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza ushiriki wa wanawake katika mnyororo mzima wa thamani katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Mamkwe ameeleza kuwa wanawake wa wizara hiyo walishiriki maadhimisho hayo kwa ufadhili wa Mradi wa Kuendeleza Usimamizi wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji wa Bahari Tanzania (TASFAM).

“Leo Wizara ya Mifugo na Uvuvi tupo Kongwa kuadhimisha siku hii muhimu katika maisha ya mwanamke kuanzia anapozaliwa hadi anapokuwa mtu mzima. Tunashukuru mradi wa TASFAM ambao umetuwezesha kufika hapa na kujumuika na wanawake wenzetu,” amesema.

Kaimu Mwenyekiti wa Wanawake wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Joyce Mamkwe akizungumza hivi karibuni wilayani Kongwa, Dodoma

Ameongeza kuwa mradi huo una programu ya kuendeleza shughuli za uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji katika ukanda wa pwani, huku wanawake wakitajwa kuwa sehemu muhimu ya jamii inayotarajiwa kunufaika na kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo.

Kwa upande wake, Teddy Salema kutoka idara ya uendelezaji wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo katika wizara hiyo, ameushukuru mradi huo kwa kuwawezesha kushiriki maadhimisho hayo.

Amesema jamii inapaswa kutambua uwezo wa wanawake kwani wakipewa nafasi na kuwezeshwa wanaweza kuleta maendeleo makubwa nchini.

“Wakati mwingine wanawake huonekana kama hawawezi, lakini wakipewa nafasi wanafanya mambo makubwa.

“Tunaona hata Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha uwezo mkubwa wa uongozi,” amesema.

SOMA: Taasisi ya Mariam Mwinyi inavyobadilisha maisha Zanzibar

Salema ameongeza kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika sekta ya mifugo, hususan katika shughuli za ufugaji, chanjo, pamoja na uzalishaji wa malisho na vyakula vya mifugo.

“Wanawake wako mstari wa mbele kupanda malisho na kuandaa vyakula bora vya mifugo, jambo linalochangia afya ya mifugo na kuongeza pato la taifa,” amesema.

Naye Katibu wa Tawi la TUGHE katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Grace Mwaisyelage, amemshukuru Katibu Mkuu wa wizara pamoja na mradi wa TASFAM kwa kusaidia kufanikisha ushiriki wa wanawake wa wizara hiyo katika maadhimisho hayo.

Aidha, amewahimiza wanawake kuendelea kuwaelimisha na kuwawezesha mabinti kwa kuwashirikisha katika shughuli za kiuchumi ili waweze kuwa viongozi na wafanyabiashara wakubwa baadaye.

“Ni muhimu kuwalea na kuwawezesha mabinti zetu, kwa kuwa wao ndio watakaokuja kuchukua nafasi zetu hapo baadaye. Waingizwe katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama ufugaji wa samaki na miradi mingine ya maendeleo,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button