Taasisi ya Mariam Mwinyi inavyobadilisha maisha Zanzibar

WAKATI wa maji kupwa katika ufukwe wa Zanzibar, wanawake huingia taratibu ndani ya maji ya joto ya Bahari ya Hindi, wakifunga vipande vidogo vya mwani kwenye kamba zilizofungwa kati ya vigingi vya mbao. Kwa familia nyingi visiwani, kazi hii tulivu lakini yenye kutumia nguvu nyingi siyo tu njia ya kujipatia kipato bali ni mhimili wa maisha ya kila siku ya familia.

Kwa miaka mingi hata hivyo, wanawake wengi walikuwa wakikabiliwa na changamoto za mavuno madogo, masoko yasiyo na uhakika pamoja na ukosefu wa mafunzo na vifaa vya kisasa. Ilikuwa wakati wa ziara zake katika jamii kama hizi ndipo Mariam Mwinyi, Mke wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi alianza kuona jinsi hatua ndogo za kusaidia jamii zinavyoweza kubadilisha maisha kwa kiasi kikubwa.

Leo uzoefu huo umegeuka kuwa dhamira pana kupitia Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), taasisi isiyo ya kiserikali anayoiongoza kama Mdhamini na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini. Akizungumza katika mahojiano maalumu na timu ya waandishi wa habari kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) nyumbani kwake Migombani, Mama Mwinyi anasema kuwa kuwawezesha wanawake si suala la haki pekee, bali pia ni njia ya kujenga familia imara na taifa lenye nguvu.

“Nawahimiza wanawake na wasichana kujiamini, kuthamini elimu na kusaidiana katika kujenga mustakabali bora,” anasema katika mahojiano hayo ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2026. SOMA: Mariam Mwinyi azindua Zanzibar Afya Week

Kutoka ziara za jamii hadi kuwa dhamira ya maendeleo.Mama Mwinyi anaeleza kuwa wazo la kuanzisha taasisi hiyo lilitokana na changamoto alizozishuhudia wakati wa ziara zake katika jamii mbalimbali Zanzibar. Moja ya matukio yaliyomgusa zaidi ni kukutana na wanawake wakulima wa mwani, ambao licha ya kufanya kazi kwa bidii walikuwa wakipata ugumu kuendesha maisha yao.Kilimo cha mwani ni shughuli muhimu ya kiuchumi Zanzibar na ni sehemu inayokua ya uchumi wa rasilimali za bahari (blue economy).

Maelfu ya wanawake hutegemea shughuli hiyo kupata kipato, lakini kwa muda mrefu wengi wao walikosa vifaa, mafunzo na masoko ya uhakika ya kuboresha uzalishaji wao. Kupitia ZMBF, Mama Mwinyi amejikita katika kuwasaidia wanawake hao kubadili juhudi zao kuwa fursa endelevu za kiuchumi. Hadi sasa, taasisi hiyo imesaidia zaidi ya wakulima wa mwani 1,400, wengi wao wakiwa wanawake, kwa kuwapatia mafunzo ya mbinu za kisasa za kilimo, udhibiti wa ubora na namna bora ya kushughulikia mwani baada ya kuvunwa.

Matokeo yamekuwa makubwa
“Wakulima wengi wamefanikiwa kuongeza uzalishaji mara mbili ikilinganishwa na walivyokuwa wakivuna hapo awali,” anasema Mama Mwinyi, akibainisha kuwa mavuno makubwa yameongeza kipato cha familia nyingi.

Taasisi hiyo pia imesaidia wakulima kujiunga katika vikundi, jambo linalowarahisishia kupata mikopo na kushirikiana na wadau wa maendeleo. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, taasisi hiyo pia imetoa vifaa muhimu, ikiwemo boti zenye injini, ambazo zinawawezesha wakulima kulima mwani katika maeneo ya maji ya kina kirefu ambako mwani hukua haraka na kuwa na ubora zaidi.

Wanawake katikati ya maendeleo
Mama Mwinyi anaamini kuwa ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi ni kichocheo muhimu cha maendeleo. “Hakuna maendeleo ya kweli bila mchango wa wanawake,” anasema. Kupitia programu zake, ZMBF inafanya kazi sambamba na vipaumbele vya maendeleo vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na malengo ya maendeleo ya kimataifa, ikiwemo Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Mipango ya taasisi hiyo inalenga zaidi katika kuwawezesha wanawake, ustawi wa watoto na maendeleo ya vijana, maeneo ambayo Mama Mwinyi anasema ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu.“Vipaumbele hivi vinaendana kwa karibu na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 pamoja na Ajenda pana ya maendeleo ya Afrika ya 2063,” anasema.

Kuwekeza maisha ya mtoto
Mbali na uwezeshaji wa kiuchumi, taasisi hiyo pia inawekeza katika ustawi wa watoto, hasa katika miaka ya mwanzo ya maisha yao. Kupitia programu za Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (Early Childhood Development – ECD), ZMBF inahamasisha ukuaji mzuri wa afya na maendeleo ya kujifunza kwa watoto kuanzia kuzaliwa hadi kufikia umri wa miaka mitano. Mama Mwinyi anaeleza kuwa miaka ya mwanzo ni muhimu sana kwa maendeleo ya ubongo na mafanikio ya elimu baadaye.

“Ikiwa tunataka kizazi chenye nguvu baadaye, lazima tuwekeze kwa watoto katika kipindi hiki muhimu cha ukuaji,” alisema. Kupitia programu za lishe na ustawi wa watoto, taasisi hiyo tayari imewafikia zaidi ya watoto 9,700, na kusaidia kuboresha afya zao pamoja na maandalizi yao ya kuanza shule.

Kusaidia wasichana na masomo

Eneo lingine la kipaumbele ni kusaidia wasichana balehe kuendelea na elimu yao.Katika jamii nyingi, ukosefu wa vifaa vya usafi wa hedhi husababisha wasichana kukosa masomo wanapokuwa katika hedhi. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, taasisi hiyo ilianzisha Mpango wa Tumaini, ambao husambaza vifaa vya hedhi vinavyoweza kutumika tena kwa wasichana wanaosoma shule.Hadi sasa, zaidi ya wasichana 7,000 wamepata vifaa hivyo.

Faida nyingine ya mpango huo ni kwamba vifaa hivyo hutengenezwa hapa hapa Zanzibar kupitia kiwanda kidogo kinachoendeshwa na taasisi hiyo, na hivyo pia kutoa ajira kwa vijana. Kila kifaa kinaweza kudumu kati ya miaka mitatu hadi mitano ikiwa kinatumika vizuri.“Hakuna binti anayepaswa kukosa shule kwa sababu ya hedhi,” anasema Mama Mwinyi.

Upatikanaji huduma za afya

Kupitia programu nyingine inayojulikana kama Afya Bora Maisha Bora, taasisi hiyo imekuwa ikipanua upatikanaji wa huduma za afya pamoja na elimu ya afya kwa jamii. Zaidi ya watu 30,000 wamenufaika na huduma na kampeni za uhamasishaji zinazohusu afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto pamoja na uchunguzi wa mapema wa magonjwa.

Huduma hizi ni muhimu hasa kwa wanawake wanaoishi katika maeneo ya mbali ambao mara nyingi hukabiliwa na changamoto ya kupata huduma za afya kwa urahisi. Ili kuimarisha athari zake, taasisi hiyo inashirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika masuala kama uhamasishaji wa lishe bora, kuzuia ukatili wa kijinsia na kuboresha afya ya uzazi.

Mama Mwinyi pia alisisitiza umuhimu wa lishe bora kwa watoto, akibainisha kuwa visa vingi vya udumavu vinahusishwa na ukosefu wa elimu kuhusu lishe bora. Anasema wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye virutubisho vinavyosaidia ukuaji mzuri wa mwili.

Kujenga ushirikiano kwa ajili ya mabadiliko
Zaidi ya Zanzibar, Mama Mwinyi hushiriki katika majukwaa ya kikanda na kimataifa yanayowakutanisha wake wa marais pamoja na watetezi wa maendeleo kutoka Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.

Majukwaa hayo huwapa viongozi nafasi ya kubadilishana uzoefu na mikakati ya kuwawezesha wanawake na kuboresha ustawi wa jamii. Mama Mwinyi anaamini kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazofanana. “Wanawake wanapoinuka, jamii huinuka na mataifa husonga mbele,” anasema, akiongeza kuwa juhudi hizo pia zinaendana na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

“Kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, “Give to Gain”, inaonesha kwamba mafanikio ya kweli katika usawa wa kijinsia yanahitaji juhudi za makusudi kutoka kwa serikali, taasisi na watu binafsi.“Tunapowekeza katika usalama, haki na uongozi wa wanawake, tunaimarisha jamii kwa ujumla,” anasema,.

Dira ya jamii imara
Kwa Mama Mwinyi, kazi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation inaakisi imani rahisi lakini yenye nguvu: kuwawezesha wanawake huimarisha familia, na familia imara hujenga jamii thabiti. Kuanzia mashamba ya mwani kandokando ya bahari hadi madarasa ya shule na vituo vya afya visiwani, mipango inayoungwa mkono na taasisi hiyo inaendelea kubadilisha maisha ya watu hatua kwa hatua.

Na wakati wanawake wa Zanzibar wanaungana na wenzao duniani kote kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Mama Mwinyi anasema ujumbe unabaki wazi. “Kuwawezesha wanawake si suala la usawa pekee bali ni msingi wa maendeleo endelevu na mustakabali bora kwa vizazi vijavyo.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button