Mama adaiwa kuua mtoto kwa kipigo

MBEYA; JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Marry Timotheo, mkazi wa Kijiji cha Garijembe Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake, Scola Mwaba (10), mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Ngonde.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo lilitokea Desemba 9, mchana katika Kijiji cha Garijembe, Kata ya Tembela, baada ya Marry kumuadhibu kwa kumpiga na kitu kizito kichwani kwa madai ya utukutu.
Amesema baada ya mama huyo kumpiga mtoto wake hadi kufa, alienda kutupa mwili wake shambani jirani na nyumba yake kwa kushirikiana na Sharifa Nzalanje, mkazi wa Garijembe na wote wanashikiliwa Polisi.
Polisi imewaomba wazazi na walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwa kutoa adhabu kali kwa watoto, badala yake watoe adhabu za kuwarekebisha na kuwafundisha mienendo na maadili mema, ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata ikiwemo kupoteza maisha au kupata ulemavu.



